Tuesday, December 5, 2017

Wananchi waelimishwe faida ya kupiga chapa mifugoPicha na mtandao.

Picha na mtandao. 

By Bakari Kiango

        Hivi sasa mchakato wa upigaji chapa mifugo, hususan ngo’mbe, chini ya uratibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, umeshika kasi.

Mchakato huu ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Miezi michache iliyopita Majaliwa alitoa agizo hilo na kuwataka watendaji kulisimamia kikamilifu na kuwataka wafugaji kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Serikali kulitekeleza.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo linalolenga kusaidia kutatua changamoto na migogoro inayojitokeza baina ya wakulima na wafugaji.

Lakini pia uwekaji chapa unasaidia utambuzi wa mifugo hiyo nchini, ili ichangie katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali za kimataifa, Tanzania ni nchi ya tatu kwa wingi wa mifugo barani Afrika ikiwa nyuma ya Sudan na Ethiopia, lakini mifugo imekuwa haina mchango mkubwa kiuchumi ikilinganishwa na wingi wake.

Upigaji chapa wa mifugo ni utekelezaji wa Sheria namba 12 ya 2010 ya usajili, utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo, inayoeleza kuwa jambo hilo litasaidia kudhibiti wizi wa mifugo, magonjwa ya mlipuko, kuhakiki usalama kwa walaji wa vyakula vitokanavyo na mifugo, ustawi wa wanyama na kuwezesha biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi.

Naipongeza Serikali kwa uamuzi huu unaolenga pia kujua takwimu kamili za mifugo iliyopo katika mikoa mbalimbali ili kuweka mikakati bora ya kukuza sekta ya ufugaji.

Pia, mpango huu unalenga kuzuia mwingiliano na mifugo inayotoka nchi za jirani.

Hata hivyo, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa wafugaji. Wengi wanafikiri uwekaji wa chapa ni mkakati wa Serikali kutaifisha mifugo yao.

Hivi karibuni nilibahatika kufanya ziara katika kijiji cha Perani wilayani Mkinga, Mkoa wa Tanga. Wafugaji wa eneo hilo walimweleza, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega kuwa hawajaelimishwa kuhusu mchakato wa upigaji chapa.

Wafugaji hao walisema mpango huo una lengo la kuwanyang’anya mifugo yao.

Maelezo yao yalimlazimisha Ulega kutoa darasa kwa wafugaji hao na kuwahakikishia kuwa Serikali haina nia hiyo.

Kimsingi, alichofanya waziri kilipaswa kufanywa siku nyingi na maofisa mifugo ambao wamejaa kila kona ya nchi yetu.

Hali hii ya kutokuwa na elimu ya kina kuhusu upigaji chapa wa mifugo itawaacha baadhi wafugaji njia panda, kwa sababu hawana uelewa kuhusu mchakato huu.

Nawashauri maofisa mifugo kuacha tabia ya kukaa ofisini, badala yake wajihimu kuwatembelea wafugaji kwa ajili ya kutoa elimu ya upigaji chapa, mchakato ambao kimsingi una manufaa kwa wafugaji. Wafugaji hawa wakielimishwa, naamini mchakato utakwenda kwa ufanisi na kukamilika ndani ya muda uliowekwa.

Naeleza haya kwa sababu katika baadhi ya maeneo niliyotembelea, wafugaji walisema kuwa hawana tatizo na upigaji chapa, ila wanaomba kuelimishwa zaidi ili kuondoa baadhi ya sintofahamu.

Aidha, ni wakati mwafaka kwa wizara husika kulishughulikia jambo hili kwa haraka, ikiwamo kuwagiza maofisa wa mifugo kuweka kambi katika vijiji na kutoa elimu, badala ya kusubiri kazi hiyo kufanywa na watendaji wakuu wa wizara kama ilivyo sasa.

Hatua hii pia itasaidia viongozi wakuu wa wizara kufanya shughuli nyingine hasa za kutatua changamoto wakati wa ziara zao, badada ya kutumia muda mwingi kutoa ufafanuzi kwa wafugaji kuhusu mchakato wa upigaji wa chapa.     

-->