Wanasiasa wasiingilie majukumu ya Tume ya Nidhamu ya Walimu

Muktasari:

  • Wanajadiliwa na kuhukumiwa bila utetezi. Utekelezaji hutakiwa kufanywa mara moja na ofisi za wakurugenzi wa halmashauri husika.
  • Hakuna mkurugenzi mwenye ubavu wa kuhoji uamuzi wa kikao cha halmashauri kuu ya chama. Badala yake walimu wamekuwa wakiumizwa kimya kimya ili kukidhi matakwa ya kisiasa ya makada wa chama.

Matukio ya adhabu kwa walimu baada ya maazimio ya vikao vya wanasiasa, ni aina nyingine ya udhalilishaji wa taaluma unaozidi kujenga hofu kwa watumishi hao wa umma.

Wanajadiliwa na kuhukumiwa bila utetezi. Utekelezaji hutakiwa kufanywa mara moja na ofisi za wakurugenzi wa halmashauri husika.

Hakuna mkurugenzi mwenye ubavu wa kuhoji uamuzi wa kikao cha halmashauri kuu ya chama. Badala yake walimu wamekuwa wakiumizwa kimya kimya ili kukidhi matakwa ya kisiasa ya makada wa chama.

Kwa mfano, Oktoba 2016, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kasamwa mkoani Geita, Dennis Otieno alikumbana na adhabu ya kuhamishwa shule. Msingi wa adhabu hiyo ulikuwa ni uamuzi uliofikiwa kupitia vikao vya chama.

Kosa la mwalimu huyo ilikuwa ni kupinga kitendo cha walimu kuwachangisha fedha wazazi wa watoto ambao ni wanachama wa klabu ya Magufuli na kuzuia wasivae sare za chama siku ya mahafali ya kidato cha nne.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Kasheku Musukuma alikiri kufanyika kwa kikao kilichotoa pendekezo la mwalimu huyo kupewa adhabu.Utekelezaji ulifanyika mara moja na hakuna sababu zozote za kitaaluma au kimaadili zilizotajwa.

Tukio la hivi karibuni ni kupigwa mabomu wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bariadi, Simiyu. Msingi wa vurugu hizo ni azimio la kikao cha halmashauri kuu ya CCM kuagiza walimu wawili wa shule hiyo wahamishwe.

Wanafunzi wa shule hiyo walifunga barabara na kuandamana kupinga kuhamishwa kwa walimu wao. Katibu wa CCM wa Wilaya ya Bariadi, Niclous Kasendamila alikiri kufanyika kikao cha chama kuagiza walimu hao wahamishwe.

Kikao chochote cha chama cha siasa si eneo sahihi la kujadili masuala ya walimu iwe ni kuhusu nidhamu yao au changamoto zinazowakabili kama watumishi wengine wa umma.

Huu ni uvamizi wa majukumu yanayotakiwa kufanywa na mamlaka zilizopo kisheria.

Ni vigumu mwalimu kutendewa haki katika vikao vya wanasiasa ambao nyuma yao huwa wamebeba ajenda za siri, ili kufanikisha malengo yao ya kisiasa na kupendekeza adhabu kwa walimu wanaoweza kuwa kikwazo kwao. Kama ilivyotokea katika sekondari za mikoa ya Simiyu na Geita, wanasiasa wenye ajenda za siri huwajadili walimu wakiwa wamebeba chuki na visasi vifuani. Hutoa adhabu za kuwakomoa lakini si kwa kuwa walimu hao ni kikwazo cha maendeleo ya kielimu.

Nguvu ya makada ndiyo iliyotumika kumng’oa aliyekuwa Ofisa Elimu wa Manispaa ya Bukoba, Edwin Fande aliyekuwa mratibu wa uchaguzi baada ya mgombea wa Chadema katika mtaa wa Omukituli, Kata ya Kibeta, kupita bila kupingwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alihukumiwa kwenye vikao vya chama. Kosa kubwa ilikuwa ni kupokea barua ya mgombea wa chama tawala aliyetangaza kujitoa, hivyo mgombea wa Chadema kukosa mshindani.

Siku ya kupiga kura jina la mgombea wa CCM halikuwepo kwenye karatasi.Viongozi wa CCM walikusanyika katika mtaa huo na kuapiza kumshughulikia kwa kuhujumu jina la mgombea wa chama chao. Ndivyo ilivyokuwa, miezi michache baadaye akahamishiwa mkoa mpya wa Katavi.

Walimu kama walivyo watumishi wengine wa umma ni sehemu ya jamii ileile wanayoitumikia. Hawatakiwi kuhukumiwa kwa hisia kuhusu utendaji wao wa kazi kupitia katika vikao vya kisiasa ambavyo havina nguvu kisheria. Walimu lazima wawe huru kwa mitazamo, maoni na misimamo kwa mambo yasiyohusiana na majukumu ya kazi zao kitaaluma. Si lazima wafungwe na misimamo sawa na wanasiasa waliopo katika maeneo yao au nje ya hapo.

Pamoja na kuwa uhamisho wanaopata baadhi ya walimu unaweza kutajwa kuwa wa kawaida, nyuma yake unakuwa na ajenda za kisiasa na kutaka kumkomoa mhusika pengine kwa kusimamia kile anachoamini.

Madiwani wanatumia nguvu kubwa kuwashitaki walimu waliopo kwenye maeneo yao ndani ya vikao, si kwa sababu wameshindwa kutekeleza wajibu wao bali kwa kuonekana ni kikwazo kutimiza malengo yao kisiasa.

Nao wakurugenzi wanaingia kwenye mitego ya wanasiasa na kuidhinisha adhabu za kuwakomoa watumishi wao.

Masuala ya utumishi na nidhamu ya walimu yabaki kwenye chombo kilichopo kisheria ambacho ni Tume ya Utumishi na Nidhamu ya Walimu(TSD), si kwenye vikao vya kisiasa. Inatakiwa iwe hivyo kwa watumishi wote wa umma.

Phinias Bashaya ni Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi mkoani Kagera-0767489094