Wanawake wenye kichocho huambukizwa ukimwi kirahisi

‘‘Jamii iwe na utamaduni wa kuondoa majani yaliyoota kwenye maji sehemu ambazo watu huenda kuchota maji, kufua na kuoga katika mabwawa, mito, maziwa, mifereji kwa lengo kuharibu makazi ya konokono. Pia watu wanapaswa kuchemsha maji ili kuuwa vijidudu vya maradhi mbalimbali ikiwemo wadudu wa kichocho, hapa tunashauri pia kuchemsha maji ya kuoga walau nyuzi joto 65 kwa muda wa dakika tano’’

Muktasari:

>>Serikali imeshauri wananchi kupima afya zao mara kwa mara

Utafiti uliofanywa kuanzia 2011 hadi 2016 na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), umebaini kuwa mtu mwenye ugonjwa wa kichocho yupo katika hatari ya kupata virusi vya Ukimwi na saratani ya kibofu cha mkojo kutokana na kinga yake kupungua.

Mtafiti Mkuu Kiongozi wa  NIMR, Dk Leonard Mboera anasema kichocho cha mkojo kwa hapa nchini, kimeenea kwa kiwango kikubwa eneo la Kanda ya Ziwa Victoria, katika Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Mara na Tabora.

Anasema kichocho au (schistosomiasis au bilharzias) ni ugonjwa ulioenea katika maeneo mengi ya Tanzania, lakini ugonjwa huu unaambukizwa na minyoo wajulikanao kama  Schistosoma na huathiri mfumo wa mkojo na uzazi.

Dk Mboera anasema kichocho cha mkojo kimesambaa karibu nchi nzima na ndicho kinachofahamika kwa watu wengi.

“Mbali na maeneo hayo, pia ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi katika Mikoa ya  Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara, ni miongoni mwa iliyoshamiri ugonjwa huu,”anasema Dk Mboera.

Anasema bila kupata matibabu  mapema, kichocho kinawaweka wagonjwa katika hatari ya kupata saratani ya kibofu cha mkojo.

Hali ikoje nchini?

Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk  Safari Kinung’hi  anasema kwa Tanzania  tatizo hilo ni kubwa.

“Karibu asilimia 55 ya watu hapa nchini  wanasumbuliwa na ugonjwa wa Kichocho. Ni wakati kwa jamii kuhakikisha wanajilinda kwa kutumia maji safi na salama,” anasema Dk  Kinung’hi. 

Anasema utafiti uliofanywa na Taasisi yake kuanzia 2011 hadi 2016 katika mikoa hiyo, unaonyesha maambukizi ya kichocho yanasababisha kupungua kwa kinga ya mwili na huchangia kwa kasi kubwa madhara ya VVU.

Dk Kinung’hi anasema kibofu cha mkojo kinapatikana sehemu ya chini ya maeneo ya tumbo na ni kiungo ambacho kina uwazi ndani ulio kama mfuko na kazi yake kubwa ni kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotolewa na figo kabla ya kutolewa nje wakati mhusika anapojisikia kukojoa.

Anafafanua kuwa kichocho cha tumbo kimeenea kandokando ya ziwa Victoria na Ziwa Nyasa na kwamba, aina zote mbili za kichocho huathiri  watoto wenye umri wa kwenda shule, wavuvi, wakulima wa mpunga pamoja na akina mama wenye umri wa kuzaa.

Anasema kiwango cha maambukizi hufikia hadi asilimia 100 kwa baadhi ya maeneo , hali aliyosema kuwa ni hatari kwa jamii inayozunguka maeneo hayo yenye kiwango cha juu cha maambukizi.

Aina ya matabaka

Kibofu cha mkojo kina tabaka tatu za tissue ambazo ni mucosa, lamina propia na muscularis.

Tabaka la mucosa ni ukuta wa ndani ambao unakutana na mkojo, tabaka hili lina kuta nyingi za seli au chembechembe zinazojulikana kama transitional epithelium cells ambazo pia hupatikana kwenye sehemu ya mirija inayojulikana kama ureters,urethra na kwenye figo.

Tabaka la lamina propia ni ukuta wa katikati ambao ni mwembamba sana kati ya kuta hizi tatu na  ambao mishipa ya damu na neva inapatikana hapo.

Tabaka la muscularis  ni ukuta wa nje ambao ndani yake kuna misuli maalumu na ndiyo ukuta mnene kati ya kuta hizo  tatu.

Kazi kubwa ya tabaka la Muscularis ni kupumzisha kibofu cha mkojo ili uingie ndani na ukishajaa, hukikaza kufanya mkojo utoke nje.

Nje ya kuta hizo tatu, kibofu cha mkojo kimezungukwa na  mafuta yanayokinga kibofu kutokana na mtikisiko wowote na kukitenganisha na viungo vingine.

Kichocho na Ukimwi

Dk Mboera anasema kwa upande wa wanawake, mayai ya minyoo ya kichocho hupenyeza katika ukuta wa kibofu cha mkojo na baadhi ya viungo vya uzazi, ikiwa ni pamoja na mirija ya mkojo, mfuko wa uzazi, shingo ya uzazi na uke.

“Katika viungo hivi, mayai hayo husababisha madhara na uharibifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na michubuko na uvimbe na kwa bahati mbaya, katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, maeneo yaliyoathirika  na kichocho ndiyo  hayohayo yenye maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi,’’ anasema Dk Mboera.

Anasema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuna uhusiano mkubwa kati ya kichocho cha mkojo na maambukizi ya virusi vya Ukimwi  (VVU) na kwamba, uhusiano huu unatokana na ukweli kuwa mayai ya minyoo ya kichocho huharibu kuta za viungo vya uzazi (hasa shingo ya kizazi)  na mfumo wa njia ya mkojo na kusababisha vidonda.

Anasema vidonda hivyo huruhusu virusi vya Ukimwi  kuingia kwenye mwili wa aliyeathirika kwa urahisi zaidi kuliko yule ambaye hana Kichocho.

“Kwa maana hii, wanawake wenye kichocho cha mkojo wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa Ukimwi  kuliko wale ambao hawana kichocho,” Anasema

Kichocho na Saratani

Dk  Kinung’hi, anasema katika maeneo yenye maambukizi ya kichocho yamechangia kuwapo kwa athari nyingine na kubwa za kiafya katika mfumo wa njia ya mkojo na kizazi.

“Athari za kichocho husababisha aina kadhaa za Saratani katika mfumo wa njia ya mkojo na kizazi na kwamba, saratani ya ukuta wa kibofu ndio inayotokea mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa,”anasema Dk Kinung’hi.

Mtafiti huyo anafafanua kuwa minyoo ya kichocho sio chanzo cha ugonjwa wa Ukimwi au saratani, lakini maambukizi ya kichocho yanamuweka muathirika katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU na saratani ya ukuta wa kibofu cha mkojo.

Dalili za ugonjwa huo

Miongoni mwa dalili za kichocho ni mkojo kuwa na damu, kujisikia mwili kuchoka, kuwa na kikohozi kikavu na maumivu ya misuli.

Kwa upande wa kichocho cha tumbo ni kuharisha kinyesi chenye damu, maumivu ya tumbo na kuvimba tumbo.

Mbali na ugonjwa huo kuwapata binadamu, pia huwapata wanyama wafugwao  kama ng’ombe, mbuzi na kondoo ambao husababishwa na minyoo iitwayo schistosoma Bovis.

Jinsi ya kujikinga

Daktari bingwa wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kutoka Kliniki ya MediCorps, Francis Makwabe anasema ni wakati kwa jamii kuacha kujisaidia haja kubwa au ndogo kwenye vyanzo vya maji hasa katika mabwawa, mito, maziwa na mifereji ya maji, kwani mtu mwenye kichocho cha mkojo anapojisaidia haja ndogo au kubwa, hutoka na mayai ya kichocho ambayo huenea katika maji.

“Watu watumie maji safi na salama yaliyowekewa dawa ya kuua vimelea vya maradhi ili kujiepusha na magonjwa mbalimbali yanayotokana na maji kutokuwa salama,” anasema Dk Makwabe.

Anasema jamii inapaswa kuacha kuoga, kuchota maji na kufua nguo kwenye maji yaliyotuama kama ya kwenye mabwawa, mito, maziwa na mifereji ambayo mingi inakuwa na konokono wanaosambaza kichocho.

Anasema jamii iwe na utamaduni wa kuondoa majani yaliyoota kwenye maji sehemu ambazo watu huenda kuchota maji, kufua na kuoga katika mabwawa, mito, maziwa, mifereji kwa lengo la kuharibu makazi ya konokono.

Hata hivyo, watu 200milioni duniani wameambukizwa ugonjwa huo, huku asilimia kubwa ya wagonjwa hao wakitoa nchi zilizo katika Bara la Afrika.

Hata hivyo, Dk Kinung’hi anasema Serikali inampango wa kutokomeza magonjwa ambayo hayajapewa kipaumbele pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na magonjwa hayo.

“Tuna wataka wananchi wajitokeza kwenda kupima afya mara kwa mara na lengo kuu ni kutaka kutokomeza kama si kuyapunguza maradhi hayo ambayo tunaweza kuyaepuka,” anasema Dk huyo.