Wasichana muonyane mimba za utotoni

Muktasari:

  • Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliochapishwa Januari 2016 umeitaja Tanzania kuwa na viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni ikiwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa asilimia 28. Hii si mara ya kwanza kutolewa taarifa za utafiti kuhusiana na tatizo hilo ambalo wasichana wengi hukatisha masomo kutokana na mimba za utotoni.

Tatizo la mimba za utotoni limekuwa likiongezeka kila mwaka na kutajwa kusababisha umaskini mkubwa katika familia na mataifa mengi katika barani Afrika.

Tatizo hili la mimba za utotoni limekuwa likichangia vifo vya mabinti wengi katika jamii zetu, kwa sababu zinaathiri afya ya muathika, pia zinawakosesha watoto hao wa kike haki ya kupata elimu na zingine anazostahili. Na pia huwapatia wakati mgumu sana watoto hao wa kuja kujijengea maisha bora ya hapo baadaye. Tukirudi upande wa sheria, tunaambiwa msichana anayebeba ujauzito akiwa na umri wa miaka 14 au chini ya hapo muhusika aliyesababisha kutungwa kwa mimba hiyo anapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwamo ya kifungo cha miaka 30 jela.

Ripoti ya mwaka 2016 ya Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (Human Right Watch) iliyopewa jina la “Nilikuwa na ndoto za kumaliza shule” inasema asilimia 40 ya watoto wameshindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya mimba za utotoni.

Utafiti huo uliofanywa na shirika hilo, unaonyesha wasichana zaidi ya 8,000 waliacha masomo baada ya kupata mimba au kuolewa kwa nguvu katika mwaka huo.

Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliochapishwa Januari 2016 umeitaja Tanzania kuwa na viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni ikiwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa asilimia 28. Hii si mara ya kwanza kutolewa taarifa za utafiti kuhusiana na tatizo hilo ambalo wasichana wengi hukatisha masomo kutokana na mimba za utotoni.

Mbali na ripoti hiyo, pia kuna mifano mingi inayoonyesha ukubwa wa tatizo kiasi cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufanya utafiti na kuutaja Mkoa wa Katavi kuwa unaongoza nchini kwa kuwa na tatizo la mimba za utotoni kwa asilimia 45.

Utafiti huo unasema mkoa huo unafuatiwa na ule wa Tabora wenye asilimia 43, Dodoma asilimia 39, Mara asilimia 37 na Shinyanga asilimia 34. Ni wazi kuwa kulingana na takwimu hizo, kuna haja ya kuongeza nguvu ya kupiga vita hali hii ili kuwanusuru mabinti zetu. Ni wazi kuwa vita dhidi ya mimba za utotoni inahitaji mikakati na sera rafiki zitakazotoa fursa za elimu pamoja na ulinzi kwa ustawi wa watoto.

Binafsi nafikiri ili kupambana na tatizo hili, ambalo kwa asilimia kubwa huwakumba watoto wanaosoma shule, kuna ulazima wa mazingira ya kujifunzia kuboreshwa.

Nasema hivyo kwa sababu watoto wengi wanasoma shule zilizo mbali na maeneo yao wanayoishi kutokana na mazingira. Hivyo, kama huduma zitaboreshwa kuna uwezekano mkubwa wa kumsaidia mtoto huyu kujiepusha na mazingira hatarishi yanayochangia wao kupata ujauzito. Zamani wengi wetu tulidhani mimba za utotoni zinawakumba zaidi watoto wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo, jambo hilo si kweli, hivi sasa hata wale walio katika familia zenye ahueni, ndipo suala la elimu ya kujitambua inatakiwa kuhamasishwa shuleni. Lakini kuna haja pia ya kuwatazama hata watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu na wale wa mitaani ambao ni waathirika wakubwa.

Kuna haja ya kuanzisha mafunzo ya ufundi stadi ili kuwanusuru watoto hao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alipokuwa akizungumza kwenye moja ya mikutano yake na wananchi, aliwaza mbali zaidi na kuwataka wasichana wabadilike. Mjema anawataka wasikubali kupata mimba za utotoni kwa kuwa zinaua ndoto zao za baadaye za kuwa na elimu na maisha bora. Mjema alipofanya mazungumzo na wanafunzi mbalimbali kwenye sherehe ya Chama cha Girl Guide (Scout), alisema wasidanganywe na vitu vidogo vidogo kama chipsi, fedha na lifti za magari au pikipiki.

Aliwaambia wakijilegeza tu, matokeo yake ni wao kujikuta wakiingia kwenye kufanya ngono zembe na kupata mimba.