Wasimulia vipodozi, rangi za midomo zilivyoathiri afya zao

Muktasari:

  • Hata hivyo, pamoja na urembo kupendwa na wengi, lakini katika upande wa pili kuna jambo linalojitokeza, je vipodozi hivyo ni salama kiasi gani?

Kujiremba ni hulka ya wanawake wengi ambao mara nyingi unaweza kuwakuta wakitumia sehemu kubwa ya muda wao wa asubuhi kwa ajili ya kujiweka sawa na kujipendezesha.

Hata hivyo, pamoja na urembo kupendwa na wengi, lakini katika upande wa pili kuna jambo linalojitokeza, je vipodozi hivyo ni salama kiasi gani?

Uthibitisho kuhusu usalama wa vipodozi hivyo umejitokeza wakati mama mmoja mwenye miaka 54 aliyetambulika kwa jina la Mariam Said alipozungumza na gazeti hili na kukiri namna ngozi yake ilivyoharibika kutokana na matumizi ya bidhaa hizo.

Anasema amekua akitumia vipodozi vya aina mbalimbali ikiwamo vile vya kung’arisha ngozi na vinginevyo. Lakini sasa ngozi yake inaonekana kama imeungua.

Hivi ni wapi Mariam alikosea?

Alianza kutumia vipodozi hivyo bila hata kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa masuala ya urembo na mara zote alifanya hivyo kutokana na msukumo alioupata toka kwa marafiki zake akiamini itamwezesha kukata kiu yake.

Hata hivyo, mambo hayakuenda kama alivyotarajia, kwani kadiri siku zilivyokatika ndivyo ngozi yake ilivyozidi kuharibika. Alipoulizwa ni wapi alikuwa akinunua vipodozi hivyo, alisema; “Wakati mwingine nilinunua kutoka kwenye maduka madogo yaani vioski ambako walidai bidhaa zao walikuwa wakipata toka nje.”

Aliongeza: “Mara zote nilikuwa nikipuuzia kuzingatia yale yaliyoandikwa kwenye lebo maana mchanganyiko wa kemikali kwenye vipodozi hivyo sikuona kuwa na tatizo kwangu na jambo nililolitilia maanani zaidi ni kutaka kupata matokeo niliyokuwa nikiyatamani.” Haya ndiyo yanayowakumba waathirika kama kina Mariam ambao mara nyingi hushawishika kutumia vipodozi kutokana na matangazo ya vyombo vya habari na hata katika mazungumzo ya kawaida kwenye vijiwe na maeneo mengine.

Kwa nini ni muhimu kujua kile kilichomo kwenye kipodozi

Mmoja wa wataalamu wa afya, Dk Mwamvua Gugu aliwahi kuzungumzia juu ya vipodozi na kusema: “Baadhi ya vipodozi ambavyo havijathibitishwa ni hatari kwa sababu vinachanganywa na kemikali zenye madhara ya muda mrefu kwa ngozi ya binadamu na vinaweza kuchukua miaka mingi kuonyesha athari zake.”

Kwa mujibu wa Dk Gugu, vipodozi vya kung’arisha ngozi hutengenezwa na kemikali za zebaki, chloroquinone na hydroquinone; ambazo wataalamu wa afya wengi hawashauri zitumike.

Akielezea namna biolojia inavyofanya kazi katika kuharibu ngozi, Dk Gugu anasema, “Ngozi yetu imetengenezwa na kitu kinachojulikana melanin ambacho kinaifanya ionekane katika uasili wake. Kuwapo kwa kemikali zozote hatarishi, kunaweza kuifanya ngozi kupoteza nuru yake na hata kusababisha maradhi ya ngozi.

Kama watu wanayajua haya, kwani wanaendelea kununua vipodozi hivi?

Utafiti uliofanywa na gazeti hili umebaini idadi kubwa ya vipodozi vinavyotumiwa na wanunuzi wengi ni vile vinavyouzwa mitaani na huuzwa kwa bei ya chini bila kuzingatia ubora wake.

Kwa mujibu wa Dk Sylvester Mathias ambaye ni ofisa mstaafu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), kuwapo kwa vitu vya kughushi vikiwamo vipodozi kunaweka afya za wananchi wengi hatarini achilia mbali suala la upotevu wa fedha.

Rangi za mdomo

Hili halina ubishi kabisa kuwa unapogusa mkebe wa mwanamke wenye vipodozi suala la kukutana na rangi za mdomo siyo kitu kigeni. Ni eneo muhimu sana kwao.

Mwanamke hawezi kuwa amekamilisha orodha yake ya vipodozi bila kuwa na urembo huo. Katika majiji makubwa likiwamo la Mwanza, kuna maduka maalumu yanayofahamika kama boutiques ambayo ni mahsusi kwa kuuza urembo wa kike.

Sophia Nyange (29) anayemiliki duka la vipodozi jijini Mwanza anasema hupata faida kutokana na biashara hiyo kwa vile sehemu kubwa ya wateja wake ni wanawake wafanyakazi.

“Kabla sijafungua biashara hii nilikuwa nikiuza nguo za watoto. Baadaye nikaja kugundua biashara hiyo ilikuwa haifanyi vizuri kama nilivyokuwa nikitaraji, hivyo rafiki yangu mmoja alinidokeza nifungue duka kwa ajili ya vipodozi vya wanawake,” anasema.

Sophia anasema huagiza bidhaa zake kutoka Nairobi Kenya, kila baada ya wiki moja. Wakati mwingine bidhaa zake za dukani huishi hata kabla ya mzigo mwingine haujaingia. “Natumia kama Sh2.5 milioni kuagiza mzigo mmoja kutoka Nairobi na hii hainipi kikwazo chochote hasa pale kunapokuwa na mahitaji makubwa kutoka kwa wateja hasa wale wa jumla ambao hulipa kabla ili wapate mzigo kama rangi za mdomo,” anasema.

Wakati kuna wale ambao kamwe hawawezi kutoka bila kwanza kujipaka rangi ya mdomo, poda sambamba na wanja, lakini wapo wanawake wengine huwa hawana tabia hiyo.

Pamela Juma (24) mkazi wa Geita, ameliambia gazeti hili kuwa amekatazwa kutumia rangi ya mdomo na daktari wake. “Miaka miwili iliyopita nilianza kutumia rangi za mdomo za aina mbalimbali, lakini hivi karibuni nilianza kutoka vipele mdomoni na ndipo dokta akanishauri kuacha kabisa kuzitumia,” anasema Pamela.

Hata hivyo, Pamela anakiri ushauri wa daktari wake. Anasema pamoja na kuacha kutumia urembo huo, midomo yake bado inapasuka na kutoa damu.

“Nadhani matumizi ya kupita kiasi yamenifanya midomo iwe dhaifu kwa vile kinga yake imepungua,” anasema mwana dada huyo.

Dhana inayotolewa na Pamela inafafanuliwa zaidi na Perpetua Hillary, mtaalamu wa ngozi mstaafu ambaye anasema rangi za mdomo mara nyingi huambatana na madhara yasiyokwepeka.

Wanawake kama Pamela huweka rangi ya mdomo mara nyingi wanapotaka kutoka nyumbani na wanaendelea na hali hiyo karibu siku nzima na hata wanapoingia kitandani.

“Kwa hali kama hii, lipustiki inaweza kukusababishia aleji, muwasho na mchubuko wa mdomo. Kiwango fulani cha kemikali yenye kuzulu pia inaweza kusababisha saratani,” anasema Dk Hillary.