Wasindikaji wa maziwa nchini changamkieni fursa hii

Muktasari:

Hiyo ni baada ya Agosti 18, Waziri Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kusaini kanuni mpya za huduma za mifugo na bidhaa zake ambazo pamoja na mambo mengine, zimeongeza tozo ya maziwa yanayoingizwa nchini kutoka Sh150 kwa kilo moja hadi Sh2,000 (sawa na ongezeko la asilimia 1,233).

Serikali imeongeza tozo ya maziwa ya nje na bidhaa zake kwa zaidi ya asilimia 1,200.

Hiyo ni baada ya Agosti 18, Waziri Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kusaini kanuni mpya za huduma za mifugo na bidhaa zake ambazo pamoja na mambo mengine, zimeongeza tozo ya maziwa yanayoingizwa nchini kutoka Sh150 kwa kilo moja hadi Sh2,000 (sawa na ongezeko la asilimia 1,233).

Kwa sasa huenda biashara hiyo ikawa na mabadiliko makubwa ama kwa maziwa yanayoingizwa kupungua na kufanya wateja wapiganie au kupanda bei kiasi kwamba wengi watashindwa kuhimili.

Tayari kanuni hizo zimeanza kuonekana tishio kwa wadau na waingizaji wa malighafi za maziwa hapa nchini wakisema hatua hiyo itasababisha wengi washindwe kumudu.

Kutokana na mabadiliko hayo, wateja waliokuwa wananunua kopo la lita moja kwa Sh3,200 kwa sasa watatakiwa kulinunua kwa takriban Sh6,000.

Wakati huohuo, viwanda vya kusindika nchini vinahitaji lita 700,000 za maziwa lakini uzalishaji uliopo ni asilimia 40, hivyo kulazimu kuagiza kiasi kikubwa kwa ajili ya uzalishaji.

Katika uagizaji huo Tanzania hutumia zaidi ya Sh165 bilioni kuagiza maziwa kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kabla ya mabadiliko ya kanuni ilikuwa ni rahisi kufanya hivyo, lakini mambo yamebadilika hivi sasa na huenda kukawa na upungufu wa maziwa nchini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza unywaji wa maziwa walau lita 200 kwa mwaka kwa kila mtu lakini takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania wanakunywa wastani wa lita 45 tu kwa mwaka, hali inayoonyesha kuwapo mahitaji makubwa

Uhai na mafanikio ya viwanda vya usindikaji maziwa, kwa kiasi kikubwa unategemea uzalishaji na upatikanaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji, jambo ambalo ni fursa kubwa, hasa endapo tutashughulika na ufugaji wa kisasa.

Tanzania kuna si chini ya vituo 17 vya serikali na binafsi vya kuzalisha ng’ombe wa kisasa. Vituo hivi vinaweza kuongezwa katika uzalishaji wa maziwa ili kukidhi mahitaji ya viwanda na soko la maziwa.

Ili kufanikisha haya, vituo vya uzalishaji na mafunzo vipewe msukumo ili kuwanufaisha wafugaji waliopo na wote wenye nia ya dhati kuanza ufugaji wa kisasa katika wilaya mbalimbali nchini.

Miongoni mwa vituo vya uzalishaji wa ng’ombe wa kisasa ni Asas, Kibebe, Sao Hill, Mabuki, Kitulo na mashamba ya utafiti ya Mpwapwa, Tanga na Uyole.

Pia, kuna vituo vingine vya Ngerengere, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Molomo, Rongai, Malonje, Sanya Juu na Dakawa.

Vituo hivyo vina ng’ombe wa kisasa wasiopungua 13,000 na endapo vikishirikishwa ipasavyo, vinaweza kuleta mapinduzi makubwa katika uzalishaji na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2018/19, Waziri Mpina alisema katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Aprili, 2018 uzalishaji wa maziwa umefikia lita bilioni 2.4 ikilinganishwa na lita bilioni 2.1 zilizozalishwa katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili, 2017.

Pamoja na hayo yote lakini uzalishaji huo bado ni kiduchu ikilinganishwa na idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia milioni 50 na mahitaji yake.

Ongezeko hili la kodi ya uingizaji wa maziwa ya nje kutawapa nafasi wasindikaji wa ndani, kutumia fursa hii kujijenga hata kushindana kimataifa katika ufugaji wa kisasa na kuanzisha viwanda vya kusindika maziwa.

Kwa upande mmoja, ongezeko hili linaweza kuwa hasara kama ambavyo imeshaanza kutajwa, lakini upande mwingine ni faida na pengine fursa ya pekee ambayo inatakiwa kuchangamkiwa na wasindikaji wa viwanda vya ndani ambalo hasa ndilo lengo kuu la Serikali.

Ni wakati sasa kuonyesha uwezo na kuhakikisha pengo hili linalotajwa na hata linaloibua wasiwasi wa kukosa bidhaa hiyo adimu linazibwa kwa kuweka mikakati endelevu na yenye matumaini kwa Watanzania.

Hatua hizi ziende sambamba na kuweka mazingira mazuri na kuhakikisha wafugaji wanapata dawa za kutosha kwa ajili ya kuogesha mifugo yao ili isidhoofu maana haiwezi kuzalisha maziwa ikiwa katika hali hiyo. pia nguvu sasa zielekezwe kutoa elimu ya kufuga kisasa.

Kiwango cha unywaji wa maziwa Tanzania bado kiko chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Nchini Kenya, kiwango hicho ni kati ya lita 19 maeneo ya mashambani hadi lita 125 maeneo ya mijini.

Jesse Mikofu ni mwanadishi wa Mwananchi mkoani Mwanza, anapatikana kwa simu namba 0755-996593