Watanzania tuseme sasa saratani basi

Muktasari:

  • Lakini hata Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni limekaririwa likisema linakadiria kuwa, kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali kwa hapa nchini.

        Tatizo la Saratani kwa Tanzania limeendelea kuongezeka kila mwaka kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

Lakini hata Shirika la Afya Duniani (WHO) hivi karibuni limekaririwa likisema linakadiria kuwa, kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali kwa hapa nchini.

Shirika hilo limesema kati ya wagonjwa hao, ni wagonjwa 13,000 tu sawa na asilimia 26 ndiyo wanaofanikiwa kufika katika hospitali kupata matibabu. Lakini Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu hivi karibuni naye amesikika akisema asilimia takribani 70 tu ndiyo hufika hospitalini kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo, alisema wagonjwa hao hufika ugonjwa wao ukiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa yaani hatua ya tatu na nne. Ukiwasikiliza vizuri matabibu wanaopima saratani, wanasema hatua hizo alizozisema Waziri Ummy si nzuri kwani hupunguza uwezekano wa mgonjwa kupona maradhi hayo.

Takwimu za mwaka 2016/2017 kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha saratani zinazoongoza nchini ni pamoja nay a kizazi kwa asilimia 32.8, saratani ya matiti kwa asilimia 12.9 na saratani ya ngozi kwa asilimia 11.7. Wataalamu hao wanasema saratani nyingine zinazoshika kasi ni pamoja nam ya kichwa na shingo kwa asilimia 7.6.

Saratani ya matezi inakuwa kwa asilimia 5.5, saratani ya damu kwa asilimia 4.3, ya kibofu cha mkojo asilimia 3.2, ya ngozi asilimia 2.8, ya macho asilimia 2.4 na ya tezi dume kwa asilimia 2.3. Katika maadhimisha ya Siku ya Saratani Duniani iliyofanyika Februari 4, Waziri Ummy alitoa wito kwa kila Mtanzania kujitokeza kupima ugonjwa huo ambao alisema ukiwahiwa unatibika. Pamoja na Serikali kuendelea kuhimiza watu tujitokeze kupima afya zetu, binafsi naona kama Watanzania wengi ni wazito. Tumeshindwa kujenga utamaduni huo na badala yake maradhi yanapotuzidia tunaanza kulalamika. Lakini kama tungewasikiliza wahudumu wa afya wanaotutaka tupime afya mapema, huenda tungesaidia kuokoa fedha nyingi tunazozitumia kusaka matibabu na pia tungeweza kuepuka vifo vya mapema.

Ifike wakati sasa Watanzania hebu tujifunze kutafuta vyanzo mbalimbali vinavyotusababishia maradhi sugu yasiyoambukiza ikiwamo saratani ili tujikinge navyo. Tukifanya hivi, kila mmoja wetu ataweza kujikinga. Kwasababu tunaambiwa vyanzo vingi vya maradhi ya saratani vinasababishwa na mtindo wetu wa maisha tulionao. Kwa mfano uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiofaa vikiwamo vile vyenye mafuta mengi, kutokula matunda na mboga mboga za kutosha, matumizi ya pombe kupita kiasi au matumizi ya dawa za kulevya na kutofanya mazoezi.

Hii yote inaepukika kwanini tusifanye hivyo ili kulinda afya zetu? Hebu tubadilike kwa faida yetu na vizazi vyetu vijavyo.

Kama kila familia itaelewa somo la kupima afya mapema na kubadili mtindo wa maisha usiosahihi, huenda tutaamsha ari na hamasa ya kutamani kujua uimara wa afya zetu kila wakati. Wakati mwingine huwa tunajaribu kutoa visingizio kuwa huduma za upimaji ziko mbali na maeneo tunayoishi, kwa kiasi fulani kisingizio hiki hakina ukweli sana hasa kwa watu wanaoishi maeneo mengi ya mijini ukiachilia mbali wale waishio maeneo ya pembezoni.

Ukichungulia takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha mwaka 2017, Serikali iliongeza vituo 1000 kutoka vituo 343 vilivyokuwapo awali kwa ajili ya huduma za kupima na matibabu katika maeneo mengi.

Vituo hivyo zikiwamo zahanati, vituo vya afya na hospitali vina vifaatiba na wtaalamu wa kutosha. Serikali inasema lengo kuu ni kutaka kuwezesha wanawake wengi kupima na kupatiwa matibabu ya awali ya saratani hasa ya kizazi na matiti ambayo inawatesa wengi wao.

Inasema imelenga kuwafikia wanawake milioni 3 nchi nzima ifikapo Desemba mwaka huu.

0713-235309