Watanzania tuzikatae kauli hizi za viongozi wastaafu

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa

Muktasari:

  • Hivi ndivyo mila, desturi na tamaduni za kiafrika zilivyo, ila nyakati zake ni kama zinapita kutokana na wale tuliowapa heshima hiyo-- kwa sababu nyepesi-- wameshindwa kutambua wajibu wao katika jamii

Tumefunzwa kuheshimu wakubwa; tuliaminishwa uzee ni ishara ya busara na hekima katika jamii.

Hivi ndivyo mila, desturi na tamaduni za kiafrika zilivyo, ila nyakati zake ni kama zinapita kutokana na wale tuliowapa heshima hiyo-- kwa sababu nyepesi-- wameshindwa kutambua wajibu wao katika jamii

Niliwahi kuandika kuwa kiongozi ni mtu anayepaswa kuwa kiungo cha kuwaunganisha watu wa rika zote katika umoja, urafiki, utu, upendo bila kujali itikadi ya vyama vya siasa, ukabila, tofauti ya uchumi, jinsia, na ukanda.

Kwa hatua hii, ndipo utulivu na amani hujengwa na watu kuwa na wasaa wa kujikita katika shughuli za maendeleo yao.

Kiongozi mwenye ulimi wa kusema lugha zinazokusudia kusababisha chuki, uadui, uchonganishi, uchochezi, uhasama wa kisiasa, kidini, kiuchumi au kikabila, hatambui nafasi yake katika jamii. Huyu anapaswa kushauriwa namna ya kuutumia ulimi vema.

Hazina bora na tunu ya Tanzania ni amani; hiki ndicho kilicho bora kuliko uchumi na siasa zetu. Mengine yote yanabaki kama mambo ya ziada.

Nazungumzia viongozi kwa kuwa ndio wenye wajibu wa mambo mengi nchini. Hatutegemei lugha za kutugawa zitolewe na kiongozi mwenye dhamana ya kuongoza umma. Maneno ya chuki au yasiyotangaza umoja wetu tuliorithi, yataligawa taifa vipande vipande.

Mwalimu Julius Nyerere aliweka juhudi za dhati kuhakikisha umoja wa kitaifa unakuwepo, ndio urithi wa kukumbukwa. Ikitokea siku yoyote tukashindwa kuilinda na kuitunza amani tuliyo nayo, kwa hakika historia ya taifa hili itapotea.

Historia ni mwalimu mzuri wa kurejelea. Mataifa mengi yaliyochezea amani, yalijikuta yakiingia katika machafuko, ambayo hayakuwa suluhu ya matatizo yao, bali yalivimbisha moyo wa kisasi, chuki na uhasama.

Viongozi hawana budi kutawala vipawa na karama za uongozi walizopewa tena kwa busara ya kiwango kikubwa.Wajikite kuheshimu utumishi kwa umma, utawala wa sheria na utawala bora.

Ubabe na matendo mabaya yapingwe, kwani kutoyakemea na kuyaacha yatakuja kusababisha taharuki. Lazima viongozi wakumbushwe mipaka yao.

Tusibebe dhana kuwa siasa ni uadui. Kutofautiana kifikira, kimawazo ni sehemu ya demokrasia. Kutofautiana huko kusisababishe wengine wabebeshwe gharama za demokrasia.

Wito wangu ni viongozi kutambua wajibu wa kulinda amani, uhai na umoja wa taifa. Wakubali ushauri na kukosolewa kwa lengo la kuboresha. Adui mkubwa wa amani ni pale tunapoona viongozi hawatendi sawa na wengi tukaamua kukaa kimya.

Nasema haya kwa kuwa sikupendezwa na kauli za Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyewaita kwa mara ya pili wapinzani kuwa ni “wapumbavu”. Alitoa kauli hii mbele ya Rais John Pombe Magufuli.

Kamusi sanifu inatoa fasiri ya mpumbavu kuwa ni sawa na juha, fala, mbumbumbu na bwege.

kwa maoni yangu kauli hii haifai kutolewa na mtu wa kariba ya Mkapa. Hakuna ushahidi wala si hekima kuwaita wafuasi wa chama fulani ni werevu na wengine ni wapumbavu, majuha au malofa.

Ni vema tukazika na kuacha viashiria vyenye nia mbaya na ovu kutoka katika vinywa vya viongozi wetu. Tuzichuje kauli, tuzichambue kwa moyo wa wema na utulivu. Kitendo cha kupokea lugha zisizofaa na kuziingiza katika matendo, matunda yake hayatalika.

Noel Shao ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. [email protected] +255769735826