Wawekezaji viwanda vya zabibu sasa waondolewa hofu Dodoma

Muktasari:

Saccos hiyo ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanachama 88 kutoka katika vijiji vya Lukali, Bankolo na Lamaiti.


Dodoma. Wakulima wa zao la zabibu wa Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) cha Lubala, kata ya Lamaiti wilayani Bahi wamewaondoa hofu wawekezaji wa viwanda na watu wanaohamia Dodoma kuwa hakutakuwa na tatizo la zabibu watakapoanza uzalishaji mwakani.

Saccos hiyo ilianza mwaka 2007 ikiwa na wanachama 88 kutoka katika vijiji vya Lukali, Bankolo na Lamaiti.

Diwani wa Lamaiti, Donald Mejitii alisema shamba wanalomiliki litakuwa likizalisha tani 1,700 kwa mwaka.

“Hizi ni tani nyingi sana ambazo hata mwanzoni tulikuwa tunaumiza vichwa kuwa tutaziuza wapi, lakini tumeamua kujenga kiwanda cha juisi,” alisema.

Mejitii ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa shamba hilo, alisema awali Saccos hiyo ilianzishwa kwa lengo la kupata mkopo wa fedha uliokuwa ukitolewa na Serikali ya Awamu ya Nne maarufu mabilioni ya JK, lakini hawakufanikiwa kupata.

“Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati huo, William Lukuvi (sasa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) alituambia tuanzishe shamba la pamoja la zabibu, wazo ambalo tulikubaliana nalo,” alisema.

Kuhusu msaada wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, alisema waliweza kuchimba kisima, kununua pampu na vifaa vya sola kwa ajili ya umeme wa jua wa kusukuma maji hayo.

Pia, alisema halmashauri iliwasaidia fedha kwa ajili ya kupima na kupata hati na kusawazisha shamba hilo ili waweze kuanza kilimo cha zabibu.

“Tulikwenda Mpango wa Kimataifa wa Chakula (WFP), wao walitusaidia chakula kwa ajili ya watu watakaochimba mitaro shambani na tukafanikiwa kuchimba mitaro 1,600,” alisema.

Alisema hatua hiyo iliwafanya kutafuta mikopo kwa ajili ya kuendeleza shamba hilo, ambapo walipata mkopo kutoka UTT Micro-Finance waliowapatia Sh275 milioni na Benki ya Uwekezaji (TIB) Sh1.3 bilioni.

“Mikopo hii ilituwezesha kuchimba kisima, kununua paneli kwa ajili ya kupata umeme mkubwa, kujenga mfumo wa umwagiliaji mzima pamoja na kuchimba bwawa kwa ajili ya kuhifadhia maji,” alisema.

Alisema fedha hizo zilipatikana Aprili mwaka jana, ambapo taasisi hizo zimekuwa zikilipia gharama za mahitaji ya shamba bila kupitisha fedha kwenye Saccos.

Hata hivyo, alisema baada ya miaka miwili ya uzalishaji taasisi hizo zitawajengea kiwanda.

Akizungumzia changamoto, Mejitii alisema ipo katika upatikanaji wa mbegu ambazo kwa mara ya kwanza walikuwa wakizipata Makutopora.

Hata hivyo, alisema kwa kuwa walihitaji mbegu nyingi, Makutopora wanaonekana kuzidiwa na ndipo waliamua kuanzisha kitalu cha kuzalisha mbegu zilizotosheleza shamba hilo.

Alisema katika kuhakikisha shamba hilo linaendeshwa kwa ufanisi, walianzisha kampuni ambayo ina Meneja wa shamba, wahandisi wa umwagiliaji na ufundi na bwana shamba ambaye hufika mara tatu kwa wiki kwenye shamba hilo.

Mejitii alisema kati ya ekari 170 za uzalishaji wa zabibu, 10 zitakuwa ni kwa ajili ya uzalishaji wa zabibu zitakazotumika kama matunda.

“Wawekezaji wa viwanda hawana haja kuhofia kuhusu malighafi, kwasababu tutakapoanza uzalishaji zabibu zitakuwa nyingi sana,” alisema.

Akizungumzia watakavyomudu gharama za uendeshaji wa shamba, Mejitii alisema mitambo yote ya maji katika shamba hilo inatumia umeme wa jua.

“Hili ni tofauti na la kule Chinangali (Wilaya ya Chamwino) ambalo limeshindwa kujiendesha kwa sababu ya gharama ya umeme imekuwa kubwa, hivyo kufanya gharama za uendeshaji kuwa kubwa,” alisema.

Skimu ya umwagiliaji ya zabibu ya Chinangali II yenye ekari 1,250 yenyewe inatumia maji yanayotoka kwenye visima na kusukumwa na mitambo inayotumia umeme wa sola, hivyo kufanya gharama za uendeshaji kuwa nafuu.

Katika shamba hilo, mmoja wa wanachama wa saccos hiyo, Idd Mlugo ambaye ni mkulima amefundishwa uendeshaji wa mitambo ya kusukuma maji kutoka katika visima hivyo na namna ya kumwagilia.

Alisema uwezo wa visima hivyo viwili, kama kuna jua la kutosha huwa ni kuzalisha lita 34,000 kwa saa.

“Jukumu langu ni kusimamia hii mitambo na kuhakikisha maji yanafika kwenye mizabibu katika mfumo wa umwagiliaji wa matone tuliofunga, mara mbili kwa wiki,” alisema.

Alisema alipata mafunzo ya wiki mbili kutoka kwa walioufunga mtambo huo na kwamba, kazi hiyo amekuwa akiifanya huku akishughulika na shamba lake la ekari mbili walilogawana kama kikundi kwenye mradi huo.

Akizungumzia changamoto, alisema walipoungana na kuja na wazo la kuanzisha kilimo cha zabibu watu wengi walijitoa na kuona jambo hilo haliwezekani.

“Wengine walijitoa kwa sababu jambo hili waliona kama mchezo wa kuigiza ambao kamwe usingewezekana, lakini baada ya kuona visima vimechimbwa ghafla wakaanza kuongezeka hadi kufikia 103,” alisema.

Mwenyekiti wa saccos hiyo, Pascal Simango alisema umoja wao una wanachama 103.

“Eneo tunalotakiwa kulima ni ekari 170, lakini eneo ambalo tumepanda ni ekari 130,” alisema.

Alisema changamoto zilizopo ni ndogo ndogo katika kilimo hicho, ikiwamo vifaa kwa ajili ya uendeshaji wa shamba hilo, kupanda na kutolingana na mchanganuo wa mradi waliouandika mwanzo wakati wanalianzisha.

Hata hivyo, alisema wanatarajia kuanza kuvuna zao hilo mwakani.

Mkulima mwingine wa zao hilo katika kata ya Mpunguzi Wilaya ya Dodoma Mjini, Jairosi Nyakapala alisema changamoto inayowakabili wakulima wa zabibu ni ukosefu wa utaalamu na mitaji.

“Wakati Serikali inafikiria kuhamia Dodoma ituongezee wataalamu wa zabibu na kuvipa uwezo vikundi vya kilimo ili viongoze tija katika uzalishaji na hivyo kutumia fursa kikamilifu,” alisema.

Alisema wakulima wengi wameshindwa kuzalisha zabibu kwa kiwango kikubwa kwa sababu hawatumii njia za kitaalamu za kulima zabibu.

“Mbolea ya kupandia inatakiwa iwe imekaa kwa zaidi ya miaka minane ili iwe imekomaa, lakini sisi wakulima hatuna uwezo wa kupata mbolea hiyo,”alisema.

Alisema analima ekari nne za zabibu, lakini uzalishaji ni tani 4.5, jambo ambalo ni hasara kwake kwa kushindwa kuzalisha kwa kiwango kinachokubalika kitaalamu.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa kilimo cha zabibu Wilaya ya Bahi, Emmanuel Olomi, zabibu huanza kuvuna baada miezi 18 mara tangu kupandwa kwa miche shambani.

Hata hivyo, kulingana na matunzo anaweza kuendelea kuvuna hadi itakapozeeka na kufa baada ya miaka 70.

Alisema mavuno ya zabibu huwa ni mara mbili kwa mwaka na kwa mkoa wa Dodoma ni Aprili na Agosti na zinastawi katika maeneo yote, isipokuwa yenye baridi.

Alisema mavuno huwa kati ya tani moja kwa ekari hadi mbili, lakini mavuno huongezeka kwa kuzingatia utunzaji wa shamba.

Dodoma ndiyo mkoa pekee unaosifika kwa kilimo cha zabibu za matunda na za kuzalisha juisi kwa ajili ya kutengeneza mvinyo.