UCHAMBUZI: Wazazi walindeni watoto kipindi hiki cha likizo

Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wamefunga shule na sasa wameanza likizo ndefu ya mwisho wa mwaka.

Ni muda ambao unawapa wanafunzi fursa ya kupumzika baada ya kuwa darasani kwa kipindi cha miezi kadhaa. Ni wakati wa kubadilisha mazingira na mawazo.

Ni muda wa wanafunzi kuwa pamoja na wazazi hasa kwa wale wanafunzi ambao wanasoma shule za bweni.

Wale wanaosoma shule za bweni wanaifurahia likizo, kwa kuwa sasa watakuwa karibu na wazazi kwa zaidi ya mwezi.

Wanaporudi nyumbani wanategemea kupata ahueni ya tofauti wa mazingira waliyoyazoea shuleni. Wanakuwa na shauku ya mambo mengi nyumbani hasa kwa vile vitu ambavyo hawavipati shuleni.

Ikumbukwe kwamba shule nyingi wanafunzi hawaruhusiwi kutumia simu za mikononi pamoja na kuangalia vitu kama filamu na burudani nyingine.

Katika kipindi hiki cha utandawazi, shauku ya wanafunzi wengi wakikaribia likizo ni kwenda kuburudika na vitu vinavyotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mathalani, wanafunzi wengi hasa wa sekondari wanakuwa na matamanio ya matumizi ya simu za mkononi ili kuingia kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Instagram na Facebook.

Kwa mazingira ya sasa, ni vigumu kuzuia matumizi hayo wakiwa nyumbani, kwa sababu hata kama mtoto hana simu anaweza kutumia simu ya mzazi kuwasiliana na marafiki zake.

Pamoja na kwamba si kitu kibaya kuwasiliana, lakini wazazi wanapaswa kuwachunga watoto wao ili wasije kupata athari hasi katika matumizi ya simu, ikiwa ni pamoja na kujisahau kufanya maandalizi ya mwaka unaofuatia.

Wazazi wanapaswa kuwasaidia kwa kuwapa miongozo nyumbani na si kuwaacha wakajiamulia kuishi vile watakavyo. Matumizi ya simu kwa kiwango cha kupitiliza yanaweza kusababisha watoto hao kuingia katika vishawishi na kujiingiza katika mambo ambayo hayana tija.

Ndio maana naamini kuwa wazazi wanapaswa kuwadhibiti watoto katika matumizi ya simu, hasa wale ambao wanatumia simu hadi usiku wa manane.

Hali kadhalika, wazazi wanapaswa kuwasimamia watoto katika kuhakikisha wanaishi katika malezi yanayorandana na jamiii, licha ya changamoto za ulimwengu wa utandawazi.

Naamini walimu shuleni pamoja na kuwafundisha masomo ya darasani, wamezingatia malezi bora, hivyo ikawe mwendelezo wa matendo mema wakiwa nyumbani.

Hakuna haja ya mwanafunzi akimaliza likizo kuwa na mabadiliko hasi kwenye maadili, kwa kuwa amepewa uhuru wa kujiamulia nyumbani.

Kwa wale wazazi wanaojua watoto wao ni wakorofi shuleni, likizo itumike kuwafunda ili kuleta mabadiliko chanya.

Aidha, wazazi wanapaswa kusimamia watoto katika mavazi, kwa kutoruhusu mavazi ambayo hayana picha nzuri katika jamii.

Sioni sababu ya mzazi kumuacha mwanawe anatoka nyumbani na nguo ambayo akipita barabarani jamii inamshangaa. Jamii inatarajia kuona wanayofanya wanafunzi wakiwa likizo yanaakisi yale malezi waliyofundishwa shuleni.

Wanafunzi wanatakiwa wawe mfano wa kuigwa katika jamii, wawe na heshima na mienendo yao iakisi maadili ya Kitanzania.

Wazazi ambao wamezoea kuwaruhusu watoto kwenda sehemu zisizoendana nao kama disko, baa na maeneo mengine kama haya, wakumbuke kuwa huko hakuwezi kuwajenga watoto wao.

Ni vyema likizo hii wakabadilika na kuwapeleka maeneo yatakayowajenga watoto kama kutembelea mbuga za wanyama, hifadhi za taifa na maeneo ambayo watajikumbusha mambo waliyojifunza katika nadharia darasani.

Nawiwa kuwakumbusha wazazi kuwa makini kipindi hiki ambacho mengi yanaweza kujitokeza kwa watoto wao wakiwa likizo.

Mzazi akiwa makini atamuepusha mtoto na vishawishi vinavyoweza kujitokeza hasa kwa wanafunzi wa kike.

Mtoto akiwa na uhuru uliopitiliza akiwa likizo, si jambo la kushangaza kusikia baada ya muda ameacha shule kwa sababu ya ujauzito.

Ndio maana naamini kuwa wazazi wana jukumu la msingi la kumlinda mtoto, ikiwamo kumpangia ratiba shabaha ikiwa kuepuka matokeo hasi ya likizo.

Pamoja na kwamba kila familia ina mfumo wake wa maisha, haimaanishi kuwa hakuna kujisahau, ndio maana natoa rai kwa wazazi kuwa makini kuwalinda watoto kipindi cha likizo.

0753590823