Sunday, June 18, 2017

Waziri atafute mbinu kuwadhibiti Ma-RC, DC

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amezungumzia tena Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inayozungumzia mamlaka ya wakuu wa wilaya na mikoa ya kuweka mahabusu watu wanaoonekana wanaweza kuhatarisha amani na utulivu iwapo watakuwa huru kwa kipindi fulani.

Hii si mara ya kwanza kwa Simbachawene kuzungumzia sheria hiyo na kuwataka wakuu wa wilaya na mikoa kuacha kuwaweka mahabusu wananchi ovyo kwa kutaka tu kuonyesha wana uwezo huo na wengine kwa kutojua matumizi ya sheria hiyo.

Wiki hii, Simbachawene alilazimika kutoa tena ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali na mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso kama Serikali ina mpango wa kubadili sheria hiyo ili kuwaondolea wakuu hao mamlaka hayo ya kuwaweka mahabusu wananchi.

Akijibu swali hilo, Waziri Simbachawene alisema sheria hiyo inatakiwa kutumika katika mazingira ambayo hayatamuweka kizuizini kwa muda mrefu.

Pia, alisema sheria hiyo isitumike kwa lengo la mkuu huyo kutaka aonekane ana mamlaka hayo, bali kumuweka kizuizini mtu anayeonekana anaweza kuahatarisha amani na utulivu au anayetenda kosa la jinai lenye madhara hayo.

Alisema sheria inawapa wakuu hao mamlaka hayo kwa kuwa ndio wasimamizi wa shughuli za Serikali katika maeneo yao, zikiwamo za ulinzi na usalama.

Hoja ya mbunge huyo wa viti maalumu inatokana na malalamiko ya wananchi, hasa wanasiasa ambao wamekuwa wakiwekwa ndani, hata kwa makosa ambayo haya hatarishi amani na utulivu na ndio maana wengi hutolewa kizuizini kabla ya muda ambao sheria inalazimisha kuwa wafikishwe mahakamani.

Matokeo yake, sheria hiyo inatafsiriwa kuwa kama fimbo ya kukomoa wananchi walio na tofauti na wakuu wa wilaya na mikoa badala ya kutumika kwa sababu za kiusalama.

Wako watumishi wa umma waliowekwa ndani kwa ajili ya kukumbushwa wajibu wao; wapo waliowekwa ndani kwa sababu ya kutofautiana kauli na wakuu wa wilaya; wapo waliowekwa mahabusu kwa sababu ya kuchelewa kufika eneo la mkutano na wapo waliowekwa ndani kwa ajili ya kuandika habari ambazo hazikuwafurahisha baadhi ya wakuu hao.

Kwa hiyo, ukiangalia kuna makosa ya kikazi ambayo yana taratibu na mamlaka yake ya kutoa adhabu; makosa ambayo chombo cha kuyashughulikia ni mahakama na makosa mengine yaliyo na utaratibu tofauti wa kuyashughulikia.

Lakini, wakuu hawa wameendelea kutumia sheria hiyo kuwasweka mahabusu wananchi, watumishi wa umma, wanasiasa na waandishi wa habari bila ya kujali maelekezo na dhima ya sheria hiyo.

Pengine Pareso ameona suluhisho ni kufanya marekebisho ya sheria hiyo kwa kudhani kuwa ina udhaifu.

Inawezekana Pareso akawa yuko sahihi kwa kuwa sheria hiyo iliundwa kwa madhumuni tofauti na mazingira tuliyo nayo leo.

Lakini, pamoja na upungufu unaoweza kuwamo kwenye sheria hiyo, bado iko wazi na inajieleza vizuri kuhusu mamlaka hayo ya wakuu wa wilaya na mikoa kiasi kwamba anayeitumia vibaya anaonekana bila ya kufanya juhudi kubwa.

Cha msingi hapa ni matumizi mabaya ya sheria na kutoheshimu sheria. Hata kama tutakuwa na sheria nzuri kiasi gani, kama tutakuwa na watu wanaoweza kuzitumia vibaya bila ya woga, tatizo litakuwa lile lile. Hata kama tutakuwa na sheria nzuri kiasi gani, lakini tukawa na viongozi wasioheshimu utawala wa sheria, tatizo litakuwa lile lile.

Cha msingi, kwa kuwa Simbachawene ndiye msimamizi wa sheria hiyo, anapaswa kuanza kuchukua hatua dhidi ya viongozi wanaotumia vibaya sheria hiyo, iwe ama kwa kuwaripoti ili wawajibishwe na mamlaka zao za kinidhamu.

-->