Yanayosababisha kupasuka kwa chupa mapema

Muktasari:

        Wiki hii nitaelezea tukio ambalo si geni kulisikia kwa wajawazito na jamii.

Wiki hii nitaelezea tukio ambalo si geni kulisikia kwa wajawazito na jamii.

Chupa kupasuka ni neno lililozoeleka katika jamii yetu likiwa na maana kitabibu kama ngozi au tando laini inayoyazunguka maji yanayomfanya mtoto aliye ndani ya nyumba ya uzazi kuelea, imepasuka na maji hayo kutoka.

Tando hii ya ngozi huweza kupasuka kiasili wakati au baada ya uchungu kuanza. Katika hatua hii si tatizo ni hali ya kawaida kujitokeza na kitabibu hujulikana spontaneous rupture of membrane.

Pia, tando hii inaweza kupasuliwa na mtoa huduma kwa baadhi ya wajawazito, kulingana na hali zao. Kwa mfano, mtoa huduma anaweza kumtathimini mjamzito, kama kuendelea kuwapo kwa ujauzito huo kunaweza kuhatarisha maisha ya mtoto tumboni.

Na kama chupa itapasuka kabla ya muda wake kufika, huenda ikawa ni tatizo la kiafya au madhara yatokanayo na hali ya ujauzito. Hivyo, leo nitalenga zaidi kwenye eneo hili.

Kupasuka kwa ngozi laini kabla ya mjamzito kupata uchungu halisi baada ya kukamilika kwa wiki 37 za umri wa mimba, kitabibu huitwa rupture of membrane (PROM) na kupasuka kwa chupa mapema kuliko kawaida kabla ya wiki ya 37 ya umri wa mimba, kwa neno la kitabibu huitwa preterm premature rupture of membrane(PPROM).

Inakadiriwa kati ya asilimia 8 hadi 10 ya wajawazito hupata PROM na asilimia mbili hupata PPROM. Hili ni moja ya tatizo linaloweza kuchangia kuzaliwa mtoto njiti.

Madhara yanayoweza kutokea kwa mjamzito yanaweza kuwapo kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Kutokea kwa tatizo hili kuna mhatarisha mjamzito na mtoto aliye ndani ya nyumba ya uzazi kupata matatizo likiwamo shambulizi kwenye ngozi laini inayomzunguko na maji maji ambayo mtoto huelea ambayo kitabibu yanaitwa Chorioamnionitis, kondo la nyumba kujipachika vibaya, kuumia kihisia, kupata matatizo wakati wa usisimuaji uchungu na kuchelewa kushikama kwa mama na mtoto.

Kwa upande wa mtoto, anaweza kuzaliwa baada ya siku saba tangu kutokea kwa PPROM, hii hutokea kwa asilimia 80 waliopata tatizo hilo.

Madhara anayoweza kupata mtoto ni pamoja na kuzaliwa njiti, kupata uambukizi mkali wa bakteria ambayo huambatana na homa kali, maji ya nyumba ya uzazi kuwa machache na kuzaliwa na kasoro usoni,

Matatizo mengine hujitokeza wakati wa kuzaliwa. Kwani anaweza kupata matatizo kwenye mapafu, kuzaliwa na miguu na mikono yenye ulemavu, kuathirika kwa ukuaji, kuchoropoka kwa kitovu na mishipa ya damu kuvujisha damu kwenye ubongo. Hali hiyo inayoweza kuchangia kupata jeraha la ubongo.

Wajawazito walio katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili ni pamoja na watumiaji wa sigara, watumiaji wa dawa za kulevya na wenye uambukizi wa viungo vya uzazi.

Dalili kubwa ni kutokwa au kuchuruzika ghafla kwa maji maji kwenye sehemu za siri za mjamzito ambayo yanaweza kusambaa mpaka katika maeneo ya mapajani.

Maji maji hayo yanaweza kutoka pale anapokohoa au kucheza kwa mtoto kunaweza kusababisha kuchoropoka kwa kitovu cha mtoto.

Sababu ya maambukizi inaweza kuwa mjamzito ameugua homa, anatokwa na maji maji yenye harufu kali ukeni na maumivu chini ya kitovu.