MAONI-Yanga ikijipanga vyema itafika mbali Afrika

Muktasari:

  • Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 huko Awassa, Ethiopia.

Yanga imetinga hatua makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kuitoa Welaytta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1.

Katika mchezo wa kwanza, Yanga ilitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 huko Awassa, Ethiopia.

Juzi, CAF ilifanya droo ya makundi ya timu zilizofuzu na Yanga kupangwa Kundi D pamoja na USM Alger (Algeria), Gor Mahia (Kenya) na Rayon Sports ya Rwanda.

Hii si mara ya kwanza kwa Yanga kuingia hatua hiyo, itakumbukwa iliitoa Esperanca Sagrada ya Angola na kufuzu hatua hiyo mwaka juzi.

Mwaka huo wa 2016, Yanga ilipangwa kundi moja na TP Mazembe (DR Congo), MO Bejaia (Algeria) na Medeama ya Ghana. Hata hivyo, haikufanya vizuri katika michuano hiyo.

Yanga imeingia tena kwenye hatua hiyo msimu huu na ujumbe wetu kwa klabu hiyo ni kuwakumbusha tu kwamba hatua ya makundi si lelemama na hata timu ilizopangwa nazo si za kuzidharau.

Kwa mtazamo wa wengi, timu ngumu katika kundi hilo ni USM Alger pekee na wengi wanadhani ya kuwa nyingine ni mchekea. Dhana hiyo ndiyo iliyoigharimu Yanga kuziona MO Bejaia na Medeama timu dhaifu kwa kuwa hazina majina na matokeo yake ndizo zilizoipa wakati mgumu zaidi katika michuano ya mwaka 2016.

Ukiiondoa timu hiyo ya Algaria, hizi mbili nyingine si ngeni, ni za ukanda huuhuu wa Afrika Mashariki na tunajuana. Yanga inapaswa kujua kuwa timu hizo si za kubeza na zilifanya kazi kubwa pia kufika hapo.

Kwa mfano, Rayon Sports iliitoa Costa do Sol ya Msumbiji, mchezo wa kwanza iliifunga mabao 3-0 na marudiano wakailaza mabao 2-0.

Gor Mahia iliifunga SuperSport United ya Afrika Kusini, bao 1-0 na marudiano Afrika Kusini walifungwa 2-1 na kufaidika kwa bao la ugenini. Supersport iliingia katika fainali za Shirikisho mwaka jana.

Wachezaji na klabu kwa ujumla, huu ni wakati wa kuelekeza fikra kwenye michuano hiyo kikamilifu na kuhakikisha inashinda mechi zote hasa za nyumbani.

Kama ilivyonufaika katika mechi ya kufuzu makundi, tunaikumbuka Yanga kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kwani hiyi inaweza kuwa silaha yake kubwa. Katika soka kuna msemo kwamba mashabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani, Yanga iitumie fursa hiyo kikamilifu kujiwekea mtaji mzuri katika mechi za nyumbani na kwenda kupambana ugenini kusaka matokeo mazuri. Inawezekana kama ilivyojitokeza katika baadhi ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wachezaji waandaliwe kisaikolojia, wajipange waelekeze mawazo yao katika michuano hiyo na kuweka rekodi ya kufika fainali na kutwaa taji hilo.

Kingine ambacho kinaweza kuwa kazi ya benchi la ufundi ni kuzisoma timu zote ilizopangwa nazo sio rahisi kwa soka ya siku hizi kufanya vyema pasi na kumsoma na kumjua mpinzani wako.

Tunatarajia kwamba kuanzia sasa benchi hilo litaanza kuwafutilia wapinzani wake kujua nguvu yao ilipo, wachezaji gani ni tishio na mifumo yao.

Hii ni fursa kwa timu na wachezaji binafsi kujiweka katika mazingira mazuri ya kibiashara. Hii ni nafasi yao yakutoka kwani hata Mbwana Samatta alionekana katika michuano kama hii mikubwa ya ya Afrika. Hakuna shaka kwamba wakitoka, watajiongezea kipato, kulitangaza taifa na kuitajirisha klabu.