Mwananchi -

Zaidi ya miaka miaka 10, mikopo elimu ya juu kwa rufaa

Thursday December 7 2017

 

By Julius Mnganga

        Inapendeza kuona Bodi ya elimu ya Juu (Heslb) imeongeza wanafunzi wanaonufaika na mikopo baada ya kutokidhi vigezo kwenye awamu ya kwanza licha ya hatua hiyo kufikirisha.

Desemba 5, bodi hiyo ilitangaza orodha ya wanafunzi 2,679 wa shahada za kwanza ambao wameshinda rufaa hivyo kutengewa Sh9.6 bilioni. Licha ya hao, kuna wahadhiri 45 ambao watapata Sh441.4 milioni.

Kusoma si anasa. Kwanza ni haki, pili uvumilivu. Wapo wanafunzi wengi wanaoshindwa kuendelea kutokana na kukosa uvumilivu licha ya kuwa na sifa za kuendelea.

Takwimu zinaonyesha wanaohitimu elimu ya msingi ni wengi kuliko wanaojiunga kidato cha kwanza. Vivyo hivyo, wanaojiunga kidato cha tano, shahada ya kwanza mpaka uzamivu.

Ingawa kuna wanaokosa vigezo vya kuendelea kutoka hatua moja kwenda nyingine, wapo ambao mfumo unawakataa. Hapa bodi ya mikopo nayo inaingia. Inawaacha baadhi ya wanafunzi wenye sifa lakini hawana fedha kugharamia masomo yao ya juu.

Si kuwaacha leo kisha kuandaa utaratibu wa kuwapa fursa hiyo siku zijazo, bila juhudi binafsi wanafunzi hao wanapoteza kabisa nafasi ya kuendelea na masomo. Hapa panahitaji tafakuri.

Hali hii imedumu kwa muda mrefu. Bodi inahitaji kutafakali. Wanaenda wapi wanafunzi hawa wanaoachwa kila mwaka? Wanafanya nini? Kuna mpango gani wa kuhakikisha wanapata nafasi waliyoikosa?

Wakato bodi inaanzishwa mwaka 2005, wapo wanafunzi waliokosa mkopo. Kwa kutumia njia nyingine, wapo waliofanikiwa kujiendeleza na kutimiza ndoto zao. Wengine waliishia hapo hata baada ya kuomba tena na tena.

Kwenye taarifa yake ya rufaa, bodi imebainisha idadi ya walioshinda rufaa na jumla ya wanafunzi wanaonufaika mwaka huu wa masomo. Haisemi iliowaacha. Inawezekana walioachwa ni wengi zaidi ya waliopata, lakini haisemi kama ina mpango wa kuhakikisha wanapata walichokikosa.

Kuwa na taifa lenye wasomi wengi hata kama hawana ajira rasmi kuna faida kwa taifa lolote duniani. Hili linaweza kufanikiwa kwa kuweka mikakati endelevu.

Waliopewa dhamana waumize vichwa kuhakikisha hakuna mwanafunzi mwenye sifa anayekosa mkopo.

Kwa waliosoma wanafahamu changamoto zilizopo mpaka anahitimu na kupata sifa za kujiunga na chuo kikuu. Ni vijana wenye malengo pekee wanaofanikisha hili, haioendezi bodi kukatisha mipango yao.

Zaidi ya muongo mmoja wa uzoefu wa kutoa huduma hiyo, si wakati wa Watanzania kuendelea kukosa mikopo hii.

Kuna kila sababu kwa bodi kujiimarisha kwa kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili isikatishe ndoto za wananchi kupata elimu ya juu.

Wenye sifa na wanaohitaji kuendelea na shahada za juu nao wakopeshwe tafauti na utaratibu uliopo sasa hivi wa kuwakopesha wahadhiri pekee.

Kwa fursa zilizopo kwenye mfumo wa elimu uliopo hivi sasa, wapo vijana wanaostahili kujiunga elimu ya juu wakiwa na chini ya miaka 18, umri mdogo kwa elimu waliyonayo kutimiza ndoto zao.

Ikilazimu, pawepo na udahili zaidi ya mara moja ili wanaokosa mkopo Novemba, kwa mfano, waombe tena kwenye udahili wa Machi, Juni au Septemba.

Julius ni mwandishi wa gazeti hili. Kwa maoni, anapatikana kwa 0717 298 276.     

Advertisement