Zana halali za uvuvi zipatikane haraka, nafuu

Muktasari:

  • Maagizo, maelekezo na miongozo mbalimbali imetolewa kwa nyakati tofauti na viongozi ili kuhakikisha zinafanyika doria na kuwakamata wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Kuna jitihada mbalimbali zinafanywa kupambana na uvuvi haramu ambao unaonekana kukithiri na kuwa tishio kwa rasilimali za Ziwa Victoria.

Maagizo, maelekezo na miongozo mbalimbali imetolewa kwa nyakati tofauti na viongozi ili kuhakikisha zinafanyika doria na kuwakamata wanaojihusisha na uvuvi haramu.

Vilevile kumefanyika operesheni kabambe ya kukamata, kuchoma na kuteketeza zana haramu zinazotumika kuvua samaki katika ziwa hilo.

Vitendo vya uvuvi haramu vinawaweka samaki, hususani sato, sangara na wengineo katika hatari ya kutoweka Ziwa Victoria.

Kutoweka kwa samaki hao kutaathiri uchumi wa nchi, ajira na kipato kwa wananchi kuanzia kwa wavuvi, wachuuzi, wasindikaji na wauzaji, lakini pia upatikanaji wa protini muhimu kwa lishe bora ya jamii.

Hata hivyo, usimamizi wa rasilimali hizi unaonekana kupwaya kwenye maeneo mengi licha ya kutumia nguvu nyingi kutoa matamko kwa watu wanaojihusisha na uvuvi huo haramu.

Wapo baadhi ya viongozi na watu wenye dhamana ya kusimamia mazao hayo ya ziwa kuhakikisha yanavuliwa kwa utaratibu unaotakiwa lakini yamekuwapo madai mengi likiwamo la viongozi kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuruhusu uvuvi huo uendelee.

Katika kupambana na vita hiyo, Serikali mkoani Mwanza ilifikia hatua ya kutumia vyombo vyote vya ulinzi na usalama kupambana navyo.

Jambo moja ambalo huenda likasababisha vita hii ikashindwa kufanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa ni kwamba nguvu zote zimeelekezwa katika kuteketeza nyavu na zana nyingine zinazotumika ziwani badala ya kuwezesha zipatikane zana halali.

Ili kukomesha jambo hilo, imefika wakati wa serikali kuweka nguvu nyingi kuhakikisha zana halali zinazotakiwa kwa shughuli za uvuvi zinapatikana kwa urahisi na gharama nafuu.

Hili si jukumu la mtu mmoja, kwa mujibu wa Sera ya Uvuvi ya mwaka 1997 na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003, majukumu ya usimamizi, uhifadhi na ulinzi wa sekta ya uvuvi ni ya wadau wote.

Wadau wa sekta ya uvuvi ni pamoja na Serikali Kuu, Serikali za mitaa, jamii ya wavuvi, wafanyabiashara ya samaki, wachakataji wa minofu ya samaki, viwanda vya kutengeneza nyavu, mashirika yasiyo ya kiserikali, madhehebu ya dini na wabia wengine wa maendeleo.

Katika kushughulika hilo, serikali inapaswa kuwaelekeza sehemu sahihi za kupata zana zinazoruhusiwa kisheria baada ya kufanya shughuli kubwa ya kuteketeza zana ambazo zinazodaiwa kutokidhi viwango.

Kama sheria inavyokataza kutokuvua samaki wachanga, hata zana zinazoruhusiwa kisheria zinatakiwa kuelezwa wazi na kupatikana kwa urahisi na kuwezesha shughuli za uvuvi endelevu kuendelea.

Ifike wakati sasa viongozi waache kufanya kazi kwa mazoea na kutumia nguvu nyingi kushughulikia tatizo kwa upande mmoja. Kwa sababu wavuvi wenyewe hawajakosa soko, haitakuwa rahisi kuacha kuvua samaki kwa kuwa soko lake bado ni kubwa.

Vilevile, operesheni hiyo inatakiwa iwatazame wote na kuuma kotekote kama ambavyo Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Luhaga Mpina aliamuru wamiliki wa viwanda vitano vya samaki jijini Mwanza kulipa faini ya Sh180 milioni baada ya kupokea samaki walio chini ya sentimeta 50.

Inadaiwa kuwa wazalishaji na wauzaji wa nyavu zenye matundu madogo zisizoruhusiwa kuvua samaki kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi wamekuwa wakifumbiwa macho na viongozi.

Ukiitazama operesheni hiyo kwa kina, ni dhahiri kuwa jitihada zaidi zinahitajika badala ya kushughulika tu na doria za wavuvi na kuteketeza zana zao ili kupambana na upungufu mkubwa wa samaki katika ziwa hilo.

Takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri) Kituo cha Mwanza zinaonyesha kuwa samaki wanaopungua kwa kasi katika Ziwa Victoria ni sato, sangara, ningu, njegere, hongwe, nembe, gogogo na domodomo (mbete).

Kupungua kwa samaki hao kumeshusha mavuno ya rasilimali hiyo ambapo takwimu hizo zinaonesha kuwa sato waliovuliwa katika ziwa hilo walipungua kutoka tani 9,709 mwaka 2014 hadi tani 3,888 mwaka 2015.

Kwa upande wa sangara, takwimu hizo zinaonyesha kuwa waliovuliwa kipindi hicho walipungua kutoka tani 125,078 hadi tani 101,571.

Kutokana na upungufu huo, mbali na manufaa ya kiuchumi kutokana na ajira, kipato kwa wananchi na kuliingizia taifa fedha za ndani na za kigeni, pia wananchi wengi wamekosa lishe muhimu ya protini kutokana na samaki na mazao yake.

Kutokana na umuhimu huo, serikali iweke miakati ya haraka kupata zana halisi zinazoruhusiwa ili shughuli za uvuvi zenye tija ziendelee.

Jesse Mikofu ni mwandishi wa gazeti hili Mkoa wa Mwanza 0755996593