Zipo njia rahisi za kuboresha maisha ya mtoto mwenye maambukizi ya VVU

Muktasari:

Kuishi na mtoto mwenye maambukizi ya Virusi vya ukimwi ni jambo linalohitaji umakini ili kumeupusha na madhara yake pamoja na magonjwa nyemelezi.

Jana ilikuwa ni siku ya ukimwi duniani, ni nafasi nzuri kwangu kutumia nafasi hii kuendelea kutoa ufahamu zaidi ili kupigilia msumari wa mapambano dhidi ya kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Kuishi na mtoto mwenye maambukizi ya Virusi vya ukimwi ni jambo linalohitaji umakini ili kumeupusha na madhara yake pamoja na magonjwa nyemelezi.

Zipo njia rahisi ambazo mzazi au mlezi anapaswa kuzifuata ili kuishi na mtoto aliyeathirika na kumsaidia kuboresha maisha yake ikiwamo kuishi maisha marefu na kufikia malengo yake.

Yapo mambo kadhaa ambayo yakifanyika yatakuwa na tija kwa afya ya mtoto mwenye VVU kwa kumsaidia kupunguza matatizo ya kiafya yatokanayo na magonjwa sugu na nyemelezi.

 

Ushauri

Mzazi au mlezi kupata ushauri nasaha toka kwa wataalam wa afya ni jambo muhimu kwani itakufanya ulifahamu tatizo na namna ya kukabiliana nalo. Elimu hiyo inakusaidia kulinda afya ya mtoto wako aliyeambukizwa.

Kama mtoto mwenye VVU alishaanza matibabu ya dawa za kufubaza makali ya VVU na dawa za kuzuia magonjwa nyemelezi, hakikisha anapata dawa bila kukosa.

Ikumbukwe, dawa hizi hutumika kwa maisha yote ya mwathirika na ndizo zinazomwongezea muda wa kuishi. Kadri mtoto anavyotumia ARV ndivyo kinga za mwili na afya huimarika.

Ushauri nasaha na kufahamu umuhimu wa dawa za ARV na ile hali ya kufuatilia matibabu ya mtoto inakusaidia kumjengea imani na dawa hizo tangu akiwa mtoto mpaka ukubwani.

Kumjenga kitabia mapema kuna faida kubwa kwani humfanya asiache kutumia dawa hata akiwa mkubwa. Kushikamana na dawa za ARVs ndiko kunakomfanya mtu kuishi muda mrefu akiwa na VVU.

Pale unapoona dalili za magonjwa yoyote ni vema kumuwahisha kituo cha huduma za afya. Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba. Watoto wenye VVU wapo katika hatari zaidi kushambuliwa na maradhi ukilinganisha na wengine.

 

Mlo kamili

Mlo kamili wenye vyakula mchanganyiko vya wanga, protini, mafuta, mboga za majani na matunda, na unywaji wa maji ya kutosha, ni muhimu kwa afya ya mtoto.

Unaweza ukajumuisha vyakula vya asili ambavyo hupatikana kwa urahisi kwenye eneo unaloishi. Si lazima viwe vya gharama kubwa. Matunda na mboga zimesheheni virutubisho na madini mbalimbali ambavyo vinasaidia kujenga kinga ya mwili.

Hivyo ni jambo la msingi mzazi au mlezi kulima bustani za mboga na matunda na si vibaya kufuga kuku wa kienyeji kwa ajili ya mayai na nyama.

Mtoto mwenye VVU ambaye tayari ni mkubwa anahitaji mapumziko ya zaidi ya saa nane kila ili kuimarisha kinga za mwili.

 

Michezo

Kwa watoto wenye umri wa miaka miwili na kuendelea michezo ya kitoto na wenzake huwafanya kuwa na mwili imara na furaha ambazo huwapa hisia chanya hivyo kumuepusha na matatizo ya kiakili.

Mpe mahitaji mbalimbali ikiwamo vifaa vya kuchezea kama vile mpira na midoli.

 

Saikolojia

Hii ni muhimu sana. Ikianzia kwa mzazi kukubaliana na hali halisi baada ya kuelewa ushauri aliopewa ni jukumu lake kumjenga kiakili mtoto wake. Mzazi au mlezi anapaswa kumkuza mtoto vizuri kwa kumuonyesha upendo na furaha.

Mfanye mtoto asijione yuko tofauti hasa atakapofikia umri wa kuanza kujitambua. Ni vizuri akawa anaelimishwa mambo mbalimbali yenye tija kwa mustakabali wa afya yake.

Baadaye ataweza kuelimika na kukubaliana na hali yake pasipo kumpa msongo wa mawazo au sonona ambayo huweza kumfanya asiwe na afya njema.

 

Elimu na malezi.

Watoto wenye VVU pia wanahitaji malezi bora kutoka kwa wazazi au walezi na jamii kwa ujumla. Watoto hawa wanahitaji kulelewa kwa kuelekezwa na kufundishwa mambo mema na mazuri kama ilivyo kwa wengine wote.

Lengo ni kuwajenga kitabia na kupata hisia nzuri, kuzungumza nao na kuwaelekeza pasipo adhabu ni jambo la msingi. Ni kawaida kwa watoto hawa kuudhika kirahisi na kukasirika.

Ni vizuri kufahamu kuwa watoto hawa wana udhaifu mkubwa ukilinganisha na watoto wengine, mfano watoto wenye VVU ni rahisi sana kupata huzuni haraka, huwa na hasira na wakali. Elimu ni haki ya kila mtoto hivyo muda wa kuanza shule ukifika wasiachwe.

 

Mazingira

Mwekee mazingira bora; ndani na nje ya nyumba vizuri ili kumfanya mtoto ajihisi mwenye utulivu wa kimwili na kiakili.

Weka mazingira safi ya mahali anapolala, anapolia chakula na anapochezea. Hakikisha mtoto anakuwa msafi; mwili na mavazi. Hii itamfanya kuvutiwa na mazingira hayo na kuyapenda.

 

Uwazi

Ni vizuri kuweka wazi tatizo la mtoto kwa watu wa karibu mfano ndugu, jamaa na marafiki katika hatua za awali. Baadaye si vibaya kuwafahamisha walimu wake.

Ingawa bado inakubalika suala la kuweka wazi linabaki kuwa ni la mtoto, wazazi na walezi. Ni muhimu kupata ushauri nasaha kuhusiana na jambo hili la kuweka wazi juu ya hali ya mtoto.

Ushirikiano

Kujenga uhusiano mwema na makundi maalumu kama wahudumu wa afya kunasaidia kupata msaada wa haraka na taarifa mpya za kujiongezea elimu ya afya ya namna ya kuishi na mtoto.

Kuwa na urafiki mwema na familia nyingine ambazo mtoto mwenye hali kama hiyo inasaidia kubadilishana mawazo na kupata matumaini na faraja. Ni moja ya nyenzo za kupambana na unyanyapaa unaofanywa na wasio na uelewa wa Ukimwi.

Ukaribu na walimu, maofisa ustawi wa jamii, washauri nasaha ni muhimu katika malezi ya kumjenga mtoto kisaikolojia.

Ikimbukwe, mwalimu ni mlezi wa mtoto anapokuwa shuleni na ofisa ustawi wa jamii ni kiungo muhimu cha mtoto huyo na jamii yake.

Makundi mengine ni viongozi wa Serikali za Mitaa na wa dini. Viongozi hawa husaidia kuielimisha jamii na kusaidia kupambana na unyanyapaa.

Ni jambo jema kumjenga mtoto kiimani ili aweze kuishi kwa matumaini. Viongozi wa dini wengi wana uelewa na wamepewa elimu juu ya Ukimwi.