Brela: Usajili wa kampuni sasa kielektroniki

Muktasari:

  • Tangazo la wakala huo lililotolewa jana linaeleza kuwa usajili wa jina la biashara, kampuni, nembo ya biashara, bidhaa au huduma pamoja na utoaji wa leseni mbalimbali unafanyika kwa njia ya mtandao. Pia, huduma nyingine baada ya usajili nazo zitakuwa zinapatikana mtandaoni.

Dar es Salaam. Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara nchini (Brela), umezindua mfumo wa kielektroniki kusajili kampuni na biashara na huduma nyingine.

Tangazo la wakala huo lililotolewa jana linaeleza kuwa usajili wa jina la biashara, kampuni, nembo ya biashara, bidhaa au huduma pamoja na utoaji wa leseni mbalimbali unafanyika kwa njia ya mtandao. Pia, huduma nyingine baada ya usajili nazo zitakuwa zinapatikana mtandaoni.

“Mfumo unawaruhusu wateja kupata huduma zote kutoka mahali walipo,” inasomeka sehemu ya tangazo hilo.

Ofis amtendaji mkuu wa Brela, Frank Kanyusi alisema kupunguza matumizi ya karatasi kwenye huduma zao, kutaongeza ufanisi kwa kuokoa muda na kupunguza gharama katika usajili wa biashara na kukamilisha masuala mengine ya msingi.

Awali, mjasiriamali alihitaji siku tatu mpaka tano kukamilisha usajili wa kampuni yake lakini kwa mfumo uliopo hivi sasa suala hilo linaweza kukamilika ndani ya saa moja.

Kwa kampuni na majina ya biashara ambayo yalisajiliwa kabla kuanza kutumika kwa mfumo huu mpya, tangazo linawataka wamiliki kuhuisha taarifa zao ili kuweka kumbukumbu sawa.

Kuanza kutumika kwa mfumo huo kunaondoa ulazima wa wananchi wa mikoani au nje ya nchi kwenda Dar es Salaam zilipo ofisi pekee za Brela.