Kampuni ya TCCIA yaorodheshwa DSE

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban

Muktasari:

  • Kampuni hiyo ilianza kuuza hisa zake za awali (IPO) Februari Mosi mchakato uliokamilika Machi 14 na ilitarajiwa kuorodheshwa Aprili 24 mwaka jana.

 Kampuni ya Uwekezaji ya Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA investment) imesajiliwa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

Kampuni hiyo ya 27 kuorodheshwa DSE, imekamilisha mchakato huo baada ya kufanikiwa kuuza hisa milioni 112.5 kwa Sh400 kila moja.

Akizindua uorodheshaji huo, leo Machi 16, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban ameipongeza kampuni hiyo kwa uwezo wake wa kusimamia michango ya wanachama walioianzisha mpaka kufikisha mtaji wa Sh30 bilioni.

"Mtaji wenu umeongezeka kutoka Sh1.97 bilioni mpaka Sh30 bilioni mwaka jana. Mmefika hapo bila kukopa wala kupata msaada kutoka taasisi yoyote," amesema Amina.

Kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye biashara ya hisa, Amina amewataka wadau kutoa elimu kwa wananchi ili kuwapunguzia mashaka waliyonayo.

Kampuni hiyo ilianza kuuza hisa zake za awali (IPO) Februari Mosi mchakato uliokamilika Machi 14 na ilitarajiwa kuorodheshwa Aprili 24 mwaka jana. Hata hivyo, kutokana na kutokamilisha utaratibu wa DSE unaotumika hivi sasa, ililazimika kusubiri mpaka leo.

Ofisa mtendaji mkuu wa TCCIA Investment, Donald Kamori amesema mapungufu ya taarifa za wanahisa wa awali wa kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1999 ndiyo yaliyochangia ucheleweshaji huo.

 

"Sasa hivi kila mwanahisa ni lazima awasilishe akaunti ya benki, namba ya simu, nakala ya kitambulisho, majina yake matatu na anuani yake miongoni mwa taarifa muhimu zinazohitajika. Zamani haikuwa hivyo...muda wote huu tulikuwa tunakusanya taarifa hizo," amesema Kamori.