
| Wananchi Bariadi walia njaa | Send to a friend |
| Monday, 04 April 2011 21:09 |
|
SERIKALI imeombwa kuwapelekea chakula wananchi wa Kata ya Kinangw’eli, Gilya na Mwaumatondo wilayani Bariadi mkoani Shinyanga ili kuwanusuru wananchi hao kupoteza maisha kwa kukosa chakula kutokana na mazao yao kukauka kwa jua. Ombi hilo lilitolewa juzi kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hizo kwa nyakati tofauti kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga ambaye yuko katika ziara ya wiki moja ya kutembelea kata za wilaya hiyo kujionea hali ya chakula sanjari na kukagua vocha za kilimo zilizotolewa na serikali kama zimewafikia walengwa. Kilio hicho cha wananchi kilifuatia siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza kusambazwa kwa chakula cha msaada katika kukabiliana na tatizo la njaa maeneo mbalimbali hapa nchini. Baadhi ya wananchi hao, Paul Jilumbi na Pambalu Lufungulo wote wakazi wa Kijiji cha Kinangweli, walisema kuwa ni vema serikali ikapeleka chakula cha msaada chenye bei nafuu ili wananchi wenye uwezo wanunuwe kabla hawajamaliza kuuza mifugo na akiba ya pesa walizoweka na hivyo chakula kuishia kwa baadhi ya watu wasio na uwezo kabisa. “Kilio chetu kikubwa wananchi wa kata hizi hatuna chakula, mazao yetu yamekauka na jua, tunaiomba msikie kilio chetu, tupatiwe mapema chakula cha msaada la sivyo njaa itatuua”, walisema. Naye mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga alisema kuwa tayari tathimini imeshafanyika ili kujua hali halisi ya upungufu wa chakula katika wilaya hiyo na kupeleka takwimu hizo Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa kwa ajili ya kusaidia maeneo yaliyokumbwa na njaa kali. |














