|
Maofisa wa Sudan Kusini wajifunza Tz |
Send to a friend |
|
Saturday, 28 January 2012 08:59 |
|
Mwandishi Wetu MAOFISA watano waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango ya Uchumi ya Sudan Kusini, umewasili nchini kwa ziara ya wiki moja ili kujifunza kuhusu ukusanyaji wa kodi. Taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam na Chuo Cha Kodi umeeleza kuwa ukiwa nchini, ujumbe huo ukiongozwa na Naibu waziri wa wizara hiyo, Dk Marial Awou Yol, utapata fursa ya kubadilishana uzoefu na maofisa mbalimbali wa wizara za Tanzania wakiwamo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Imeeleza kuwa ziara ya ujumbe huo wa Sudan Kusini, inafuatia kumalizika kwa mradi mkubwa wa kuwajengea uwezo maofisa wa kodi katika majimbo matatu kati ya kumi ya nchi hiyo uliotekelezwa na Chuo cha Kodi cha Tanzania kwa miezi sita iliyopita.
Naibu waziri huyo na ujumbe wake pia watapata nafasi ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha , Mustafa Mkulo na Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitillya pamoja na kufanya mazungumzo ya kina na uongozi wa chuo cha kodi.
Lengo la mazungumzo hayo limeelezwa kuwa ni kuangalia uwezekano wa chuo hicho kutoa nafasi za mafunzo kwa maofisa wa kodi wa Sudan Kusini.
Sudan Kusini ni taifa jipya lililojitenga rasmi kutoka Sudan Julai 9 mwaka 2011 na sasa lipo katika mkakati wa kujenga uwezo wa kukusanya mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali visivyo vya mafuta ili kupunguza utegemezi mkubwa kwa mafuta.
|