
| Serikali yataka VETA kudahili maradufu | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 08:38 |
|
VYUO vya Elimu ya ufundi nchini (VETA), vimetakiwa kuongeza mara dufu idadi ya wanafunzi inaowadahili kwa mwaka ili kusaidia Serikali kufikisha idadi ya wataalamu 635, 000 ifikapo mwaka 2025 Naibu Katibu Mtendaji Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, Clifford Tandari alitoa agizo hilo wakati wa mkutano na wanafuzi wa Kitanzania waliosoma nchini Japan kwa msaada wa Asasi ya Shirikisho la Maendeleo nchini Japan (JATA). Alisema kuwa Serikali imekuwa ikipata wataalamu wachache kwa mwaka huku mahitaji yake ywa kipindi hicho yakiwa wataalamu 635,000 kutoka katika vyuo vya ufundi nchini. Tandari aliwataka vijana kuchangamkia nafasi hiyo ili waweze kupata fursa hiyo akieleza kuwa Serikali imetoa ruzuku kwa vyuo vya ufundi nchini. Alifafanua kuwa kutokana na ruzuku hiyo vyuo hivyo vinatakiwa kutoza Sh 60,000 kwa mwanafunzi anayesomea ufundi kwa nafasi ya kutwa na Sh 120,000 kwa mwananfunzi wa bweni badala ya kulipia 800,000 au 1,000,000 ilivyokuwa awali. Naibu Katibu huyo alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya mipango ya Serikali wamefungua milango kupitia soko huria la Afrika Mashariki (EAC), ili walimu kutoka katika nchi za Kenya, Rwanda na Burundi kuingia Tanzania na kusaidia kuziba pengo la walimu katika masomo hisabati na sayansi. Alisema kuingia kwa walimu hao nchini kutatoa nafasi kwa wanafunzi waliopo shuleni kupenda masomo ya sayansi ambayo alisema yanampa mwanafunzi nafasi ya kujiunga na vyuo vya ufundi ili baadaye nchi iweze kufikia wastani mzuri wa wataalamu. Awali akizungumza katika mkutano huo Kaimu Mwenyekiti wa JATA Dk Peter Matesa alisema lengo la kukutanana kwao ni kutaka kujadili mada mbalimbali zinazolenga masuala ya ufundi stadi na namna ya kuboresha ufundi ili kupambana na umsikini. |














