
| Gallawa afurahishwa na uzalishaji PPTL | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 08:42 |
|
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa ameeleza kuridhishwa kwake na utendaji kazi katika kiwanda cha kutengeneza mifuko ya plastiki cha PPTL na kuvitaka viwanda vyengine kuiga mfano wa kiwanda hicho. Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo jana alipotembelea kiwanda hicho katika ziara yake ya kutembelea viwanda vya uzalishaji mali vilivyopo mkoani hapo. Alisema kwamba ushirikiano mzuri aliouona baina ya uongozi wa kiwanda hicho na wafanyakazi umekiwezesha kuongeza uzalishaji na kuvuka malengo waliojiwekea. Awali akitoa taarifa ya kiwanda hicho kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkurugenzi mtendaji Jonathan Lane alisema kiwanda kinakabiliwa na wingi wa masoko kutoka ndani na nje ya nchi. Alisema mbali ya changamoto ya kutotosheleza masoko lakini pia kinakabiliwa na tatizo la upungufu wa nishati ya umeme pamoja na wafanyakazi wasio na ujuzi wa kuendesha mashine. “Tatizo la kupungua nishati ya umeme kiwandani hapa, limekuwa likisumbua siku hadi siku na kusababisha kiwanda kushindwa kufanyakazi kwa malengo,” alisema Lane. Mkurugenzi huyo alisema kuwa kiwanda hicho ambacho kinazalisha mifuko ya karatasi, Plastik na Pocylene ambayo huuzwa kwenye makampuni mbalimbali ikiwemo viwanda vya saruji. Aidha alibainisha kuwa masoko mengine ni yale kutoka nchi za Malawi, Uganda, Kenya, Zambia pamoja na Msumbiji. Naye meneja wa uzalishaji, Dominic Mkemengwa alisema kuwa kiwanda hicho kimeongeza mashine 37,mpya za kushona mifuko kutoka idadi ya awali ya mashine 90, lengo likiwa kuongeza uzalishaji kiwandani hapo. “Kutokana na kuongeza mashine hizo za kisasa hadi kufikia mashine 127, kiwanda kimefanikiwa kuongeza uzalishaji na kukidhi soko la ndani ambapo jitihada zinafanywa kutosheleza soko la nje.Hata hivyo kiwanda cha PPTL kilicho anzishwa mwaka 1995, kina jumla ya wafanyakazi 1,500. |















Comments