|
CWT kutoa tamko utata wa malipo ya walimu |
Send to a friend |
|
Saturday, 04 February 2012 08:44 |
|
Gedius Rwiza CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT),kimesema kuwa Jumatatu ijayo kitatoa tamko kuhusu utata unaoendelea katika ulipaji wa madai ya walimu sehemu mbalimbali nchi.
Hatua hiyo ya CWT imekuja baada ya walimu wengi kuilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwalipa fedha zao kama walivyohakikiwa jambo ambalo limesababisha baadhi ya walimu kufanya mgomo, ambapo walimu 54 wa Halmashauri ya Rungwe wamefutwa katika orodha ya malipo hayo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Rais wa CWT,Gratian Mukoba alisema kuwa kikao cha Baraza la CWT kilifanyika mwishoni mwa mwezi Januari na kwamba walikuwa wakisubiri kuendelea kukusanya taarifa za ulipaji wa fedha hizo na kwamba hadi sasa kuna malalamiko mengi kutoka halmashauri mbalimbali.
“Ni kweli hali sio nzuri katika mchakato mzima wa ulipaji wa fedha za walimu ambazo Serikali ilikubali kuanza kuzilipa. Tunapokea malalamiko mengi na baadhi ya walimu wanafutwa katika orodha ya malipo wakati Serikali ilituma fedha hizo kulingana na uhakiki ilioufanya, lakini kuna watu wengine wanaojitokeza kuvuruga mchakato huo,”alisema Mukoba. Wakati hayo yakiendelea uongozi wa CWT Manispaa ya Ilala umeilalamikia Serikali kwa kuwapelekea walimu fedha pungufu ikilinganishwa na idadi ya walimu wanaotakiwa kulipwa.
Katibu wa CWT, Manispaa ya Ilala James Manyama alisema kuwa shule za msingi zilitakiwa kupata Sh 193 milioni lakini wamepelekewa Sh120 milioni ambazo ni za likizo kwa walimu ni 836.
Alisema kuwa kwa upande wa shule za Sekondari Sh61 milioni zimefikishwa kwao badala ya Sh131 jambo alilosema linawapa mtihani mgumu.
|
Comments