
| TIC yataka kilimo kimarishwe nchini | Send to a friend |
| Thursday, 02 September 2010 22:12 |
|
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Emmanuel Ole Naiko amesema kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa kuendeleza sekta ya kilimo, ni vigumu uchumi wa nchi kukua kwa asilimia kati ya nane na kumi kwa mwaka. Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya wahandisi yanayofanyika kila mwaka, ambapo mpango wa Kilimo Kwanza ulizungumziwa. “ Kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa kuendeleza sekta ya kilimo, ni vigumu uchumi wa nchi ukakua kwa asilimia kati ya nane na kumi kwa mwaka,’’ alisema Naiko. Alisema hali hiyo inatokana na zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania kuwa wakulima. “ Kama wakulima wetu hawatapata bei nzuri ya kuuzia mazao, kipato chao kitazidi kushuka hivyo itakuwa vigumu, kuondokana na umaskini,” alisema Naiko ambaye pia ni makamu wa rais wa umoja wa vituo vya uwekezaji duniani . Alifafanua kwamba kilimo cha mashamba makubwa ya biashara kwa kiasi kikubwa ndicho kitaiwezesha Tanzania na pamoja na nchi za Afrika kwa ujumla, kushindana na wakulima wa nchi za magharibi ambao wanapata ruzuku kutoka serikalini. “Kulingana na hali ya uchumi wetu ulivyo sasa, hatuwezi kumudu kutoa ruzuku kwa wakulima wetu, ili tupiganie kuwepo katika biashara hasa katika kipindi hiki cha utandawazi, ni lazima tuwe na wakulima wakubwa ili waweze kushinda na wenzao wa nchi nje,’’ alisema. Mwaka mmoja sasa umepita tangu kuzinduliwa kwa mpango wa Kilimo Kwanza, ambapo katika mwaka wa fedha 2010/11, bajeti ya kilimo imepanda kwa asilimia 8.1 na kufikia Sh11.1 trilioni. Bajeti kwa ajili ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji imeongezeka kutoka Sh21 bilioni mwaka 2009/10 hadi Sh23 bilioni mwaka 2010/1.1 Tayari hadi sasa serikali imefanikiwa kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 264,388 mwaka 2005 hadi 331,490 mwaka 2010. |













