Wanafunzi 10,000 wajiandikisha na masomo ya ufundi ya VSOMO

Meneja Miradi Airtel Tanzania Jane Matinde akizungumza wakati wa semina kwa vijana kuhusu umuhimu wa kusoma kwa kutumia mtandao kupitia aplikesheni ya VISOMO inayotumiwa na VETA kwa kushirikiana na Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel katika makao makuu ya kampuni hiyo Morocco, Dar es Salaam.

Muktasari:

Kuwepo kwa teknolojia kumewezesha kuwafikia vijana wengi zaidi ambao awali walikosa nafasi ya kwenda vyuoni kujifunza

Dar es Salaam. Mpango wa kutoa mafunzo ya ufundi kupitia aplikesheni ya simu za mkononi unaoendeshwana kampuni ya Airtel kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mafunzo ya ufundi Stadi (VETA), umewavutia takribani wanafunzi 10,000.

Wanafunzi hao tayari wamejiandikisha kwa ajili ya  masomo ya ufundi stadi kupitia application ya VSOMO.

Chini ya utaratibu huo, wanafunzi hao wataweza kusoma kozi mbalimbali za ufundi.

Akiongea jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu program hiyo, Kaimu Mkuu wa chuo cha ufundi cha VETA kituo cha Kipawa, Harold Mganga amesema kuwa mafunzo ya ufundi ya muda mfupi yamekuwa yakitolewa na katika vyuo cha VETA kwa miaka mingi.

“Kwa kushirikiana na Airtel kupitia teknolojia hii tutazidi kupanua wigo na hivyo idadi ya wanafunzi kuongezeka. Itasaidia pia kupata wanafunzi kutoka sehemu za pembezoni ambako hakuna vyuo,” amesema.

Mpaka sasa wanafunzi 9,975 wamejiandikisha kupata mafunzo hayo na zaidi ya watu 33,000 wameshapakuwa aplikesheni hiyo ya VSOMO kupitia simu zao za mkononi.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa VSOMO kutoka Airtel, Jane Matinde, amesema: “Tuna mikakati mingi mwaka huu itakayowezesha watanzania wengi hususani vijana kuvutiwa na kujiunga na masomo haya ikiwemo kuongeza idadi ya kozi, kutoa elimu kwa umma juu ya upatikanaji wamasomo haya, vilevile  kutanua wigo wa upatikanaji wa huduma hii na kuboresha malipo ya ada pamoja na mikakati mingi zaidi.”