Mkuu wa mkoa ashtukia mchele kuwekewa ‘lebo’ za mikoa mingine

Muktasari:

  • Dk Kebwe alionyesha kukerwa na hali hiyo wakati akizungumza kwenye warsha ya siku mbili ya kongamano la wajasiriamali lililoandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), ambapo alilitaka kusimamia uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo ili mpunga unaozalishwa ukobolewe, ufungashwe na kuwekewa lebo za Mkoa wa Morogoro.

Morogoro. Ushindani wa biashara na masoko umemfanya mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe kuhoji baadhi ya wafanyabiashara wa mchele kununua mpunga, kuukoboa, kuuweka kwenye mifuko na kisha kuubandika ‘lebo’ zinazoonyesha umetoka mikoa mingine.

Dk Kebwe alionyesha kukerwa na hali hiyo wakati akizungumza kwenye warsha ya siku mbili ya kongamano la wajasiriamali lililoandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), ambapo alilitaka kusimamia uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vidogo ili mpunga unaozalishwa ukobolewe, ufungashwe na kuwekewa lebo za Mkoa wa Morogoro.

“Ni jambo la aibu sana wakulima wa Morogoro wanazalisha mpunga halafu wafanyabiashara wanakuja kuununua, wanakoboa mchele na baadaye wanaweka lebo za mikoa mingine ilhali ya kuwa upo uwezekano wa kuwa na viwanda vyetu vya kukoboa na kufungasha hapa Morogoro,” alisema.

Meneja wa Sido mkoani hapa, Jacqueline Mbawala alisema wamepanga kuhakikisha Morogoro inakuwa na viwanda 100 kwa kuendesha mafunzo na kutoa mikopo ya vikundi na mtu mmoja mmoja.

Kwa upande wake, meneja wa huduma za ufundi wa shirika hilo, Kalumuna Benedicto alisema wanawahamasisha wanawake kushiriki na kuwa wamiliki wa shughuli za uzalishaji mali kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji hadi Taifa badala ya kuwa wasaidizi.

Mwenyekiti wa kongano la wasindikaji wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Gaudensia Donat alisema ubora mdogo wa malighafi hasa bidhaa za vyakula unatokana na baadhi ya wakulima kutokuwa na elimu ya namna ya kuzalisha na kuhifadhi malighafi hizo.