Serikali, sekta binafsi kuzindua mabaraza

Muktasari:

  • Naibu katibu mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoljia, Profesa James Mdoe alisema mkakati wa Taifa wa kuendeleza ujuzi utashirikisha sekta binafsi kupitia mabaraza ya ujuzi yatakayoanzishwa kujadili kwa kina namna ya kuondokana na uhaba wa wataalamu nchini.

Waweka mkakati wa miaka kumi kuwapatia vijana ujuzi

Dar es Salaam. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wamedhamiria kuongeza tija katika sekta ya ajira ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hasa kipindi ambacho Serikali imetangaza Tanzania ya viwanda.

Naibu katibu mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoljia, Profesa James Mdoe alisema mkakati wa Taifa wa kuendeleza ujuzi utashirikisha sekta binafsi kupitia mabaraza ya ujuzi yatakayoanzishwa kujadili kwa kina namna ya kuondokana na uhaba wa wataalamu nchini.

“Sekta binafsi na Serikali wanalo jukumu kuhakikisha vijana wetu wanapata ujuzi ili wawekezaji wanapokuja wasipate tabu kupata wafanyakazi wenye tija. Sekta binafsi kazi yao kubwa ni kutuletea maoni kutokana na walichobaini kwenye jamii kupitia mabaraza yao,” alisema Profesa Mdoe.

Akizungumza kwenye warsha ya kuendeleza na kukuza ujuzi lililoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Profesa Mdoe alibainisha kukosekana tija katika ukuaji uchumi katika mataifa ya Afrika kwa sababu ya kutokuwapo vijana wabunifu katika utendaji.

Alisema kazi ya sekta binafsi itakuwa kuziba ombwe kati ya waajiri na waajiriwa kwa sababu watu wenye ujuzi ndiyo wanaohitajika kipindi hiki cha kuendea uchumi wa kati.

“Mataifa ya Afrika yanakua kwa kasi, lakini ukuaji huo hauendani na mabadiliko ya hali za uchumi kwa wakazi wake, sayansi, teknolojia na ubunifu vinakosekana kwa vijana wanaomaliza masomo, lazima tujiulize tatizo liko wapi. Wanakuja wawekezaji wengi lakini wanakosa wafanyakazi wenye ujuzi hivyo wanalazimika kuagiza kutoka nje,” alisema Profesa Mdoe.

Naye mkurugenzi mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema vipo vitu vingi ambavyo Watanzania wanakosa katika ajira ikiwamo ujuzi, vipaji, lugha ya Kiingereza na imani potofu kuwa Watanzania hawana uwezo kwenye ajira.

“Tanzania ina nafasi kubwa ya kukua kiuchumi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo lazima tuwe na vijana wenye ujuzi na kuwa na nafasi kubwa katika ajira. Tuwe na vitu vya ziada ambavyo viko nje ya mitalaa ya elimu tuliyo nayo sasa,” alisema.

Simbeye aliweka wazi kuwa kila mmoja anayo kazi ya kufanya kuhakikisha ujuzi katika kazi unafikiwa kama ajenda iliyofikiwa kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Haiwezekani kupiga kelele katika masuala ya miundombinu na mengine ya maendeleo halafu tunasahau kitu muhimu kama ujuzi. Mpango huu wa miaka 10 utakapokamilika mwaka 2026, tutakuwa taifa lenye miundombinu imara na watu wenye ujuzi,” alisema Simbeye.

Mkurugenzi wa ajira kutoka ofisi ya Waziri Mkuu (Ajira, Ally Msaki alisema bila elimu nzuri itakayozalisha vijana wenye ujuzi Tanzania ya viwanda itabaki kuwa ndoto.

“Kupitia mabaraza ya ujuzi tutahakikisha tunapata maoni kutoka sekta mbalimbali zinazozalisha ajira nyingi kwa sasa. Tutambue ukizungumzia ajira unazungumzia ujuzi,” alisema Msaki.