CRDB yalia kanuni mpya za uhasibu zachangia kupunguza

Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei akizungumza na wanahabari jijini Arusha juzi kuhusu mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa utakaofanyika leo na kesho katika ukumbi wa AICCC. Kushoto ni meneja masoko wa benki hiyo, Jadi Ngwale. Na Mpigapicha Maalumu

Muktasari:

Yadaiwa zimeipunguza faida kwa mwaka jana

Arusha. Baada ya kukopesha zaidi ya Sh3 trilioni, Benki ya CRDB imepata faida ya Sh36 bilioni mwaka jana ikipungua kutoka Sh63.7 bilioni iliyopata mwaka 2016.

Taarifa hiyo ilibainishwa na mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei juzi alipokuwa akizungumza kuhusu mkutano wa 22 wanahisa wa benki hiyo unaoanza leo jijini hapa.

Dk Kimei alisema faida hiyo imepatikana kutokana na maboresho ya huduma mbalimbali zinazotolewa kwenye matawi 262 yaliyopo nchini na mashine 534 za kutoa fedha (ATM).

“Kwa ujumla hali ya benki ni nzuri na tunawaomba wanahisa wote zaidi ya 1,500 wahudhurie mkutano mkuu na semina maalumu itakayofanyika Mei 18. Faida ya mwaka jana (Sh36 bilioni) unaweza kuiona ndogo ukilinganisha na tulivyokuwa tunapata awali, lakini bado ni fedha nyingi na tunaamini mwaka huu tutapata faida kubwa zaidi,” alisema Dk Kimei.

Kilichochangia kupungua kwa faida ya benki hiyo kwa miaka miwili iliyopita, ni kulazimika kuweka tengo kubwa la Sh153 bilioni za mikopo chefuchefu kutokana na matakwa viwango vya kimataifa vya uhasibu (IFRS9), kama isingetengwa wangepata faida zaidi ya Sh200 bilioni.

“Kwa sasa kanuni hizo zinahitaji kutenga uwezekano wa mkopo kutolipika hata kama haujachefuka. Katika mazingira hayo tulilazimika kupunguza faida,” alisema.

Pamoja na kuzingatia kanuni hizo, benki hiyo ilikopesha Sh3 trilioni na mkurugenzi huyo akasema inaendelea kufanya hivyo tena kwa punguzo la riba.

Wiki iliyopita, benki hiyo ilitangaza kupunguza riba kwa wafanyakazi inaowakopesha kutoka asilimia 21 mpaka 17 na kuongeza muda wa marejesho mpaka miezi 84.

Kwenye mkutano ulioanza jana, wanahisa wataongezewa ufahamu kuhusu uwekezaji katika hisa na fursa mbalimbali zinazopatikana ikiwamo namna ya kurithishanana mwenendo wa uchumi wa dunia kwa ujumla.