NMB yaombwa kusaidia gharama kuipanga Ilemela

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker

Ilemela. Wakati Benki ya NMB ikijipanga kuwafikia wakulima wengi zaidi wa pamba mkoani Mwanza, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Ilemela, John Wanga ameiomba isaidie upimaji wa viwanja kukabili makazi holela.

Wanga alitoa ombi hilo wakati wa uzinduzi wa tawi la 13 la benki hiyo jijini Mwanza linalofanya matawi yote kufika 224.

Hivi karibuni, Serikali ilitoa agizo kwa malipo ya wakulima wote wa pamba kufanyika kupitia benki ili kupunguza wizi na utapeli wanaofanyiwa na baadhi ya wanunuzi.

Naye mkuu wa idara za biashara wa NMB, Abdulmagid Nsekela alisema tawi hilo litawapunguzia wakulima kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za benki.

“Tumewarahisishia wakulima na wanunuzi wa pamba, ni utekelezaji wa agizo la Serikali la malipo yote kufanyika kupitia benki,” alisema.