Thursday, December 7, 2017

Ajira gesi, mafuta zageuka tatizo kwa wahitimu

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

       Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuwekeza kupata wataalamu wengi wa sekta ya mafuta na gesi, ukosefu wa ajira umeanza kujitokeza.

Hali hiyo inatokana na kasi ndogo ya ukuaji wa sekta hiyo ambayo inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuchangia katika uchumi siku zijazo. Hayo yameelezwa na kiongozi wa uwezeshaji wa kampuni ya Statoil Tanzania, Profesa Richard Rwechungura wakati wa mahafali ya nne ya programu ya elimu ya juu katika masomo ya mafuta na gesi inayohusisha wanafunzi wa Tanzania na Angola (Anthei).

Programu hiyo inaedeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Teknolojia cha Norway inayodhamiwa na Statoil. Profesa Rwechunguza alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepeleka wanafunzi nje ya nchi kuongeza umahiri katika fani hizo, lakini wanaporudi wanakumbana na changamoto ya kukosa ajira na sehemu za kufanyia mazoezi kwa vitendo.

Mmoja wa wahitimu Albarto Cheru alisema Serikali haijafanya maandalizi ya kutosha kuingia kwenye sekta ya mafuta na gesi.

“Huku kwenye mafuta na gesi mambo bado hayajakaa sawa ila naona Serikali inaendelea kufanya jitihada kuhakikisha tunakaa kwenye mstari,” alisema.

Naibu mkuu wa UDSM anayeshughulikia tafiti, Profesa Cuthebert Kimambo aliwataka wahitimu hao kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kwa masilahi ya Taifa.

Meneja mkazi wa Statoil, Oystein  Michelsen alisema watahakikisha Tanzania inashiriki kwa njia yoyote katika biashara ya mafuta na gesi duniani.     

-->