Asilimia 50 ya Watanzania hawajui kiwango cha fedha wanachotumia kwa wiki

Muktasari:

  • Matokeo ya utafiti wa awamu ya nne wa Financial Sector Deepening Trust (FSDT) yaliyotolewa jana, yanaonyesha watumiaji wa huduma hiyo nchini wameongezeka hadi asilimia 65 kutoka asilimia 58 miaka minne iliyopita.

 Licha ya kuongezeka kwa wananchi wanaotumia huduma za fedha, utafiti unaonyesha nusu ya watu wazima hawafahamu kiwango cha fedha walichotumia wiki iliyopita.

Matokeo ya utafiti wa awamu ya nne wa Financial Sector Deepening Trust (FSDT) yaliyotolewa jana, yanaonyesha watumiaji wa huduma hiyo nchini wameongezeka hadi asilimia 65 kutoka asilimia 58 miaka minne iliyopita.

Hata hivyo, ripoti hiyo inabainishaL “Asilimia 50 hawafahamu fedha wanazotumia kwa wiki moja iliyopita.”

Kuongezeka kwa wanaopata huduma za fedha, hakujawasaidia wananchi wa vijijini ambako maskini na wakulima wengi wanapatikana.

Wakati zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wakiishi vijijini na kutegemea kilimo kwa kipato chao, ni asilimia tatu pekee wana hatimiliki za ardhi waliyonayo.

Kutokana na kutokuwa na uhakika wa kipato, asilimia 56 ya wananchi 10,000 walioshiriki utafiti huo walisema hupunguza matumizi yao wanapohisi kuishiwa.

Utafiti huo ni wa nne ikiwa ni zaidi ya miaka 10 tangu ulipotolewa wa kwanza mwaka 2006, ukifuata mwingine mwaka 2009 na 2013.