Azania kuwasitiri kwa mikopo wanachama wa NSSF nchini

Mkurugenzi mtendaji wa Azania benki, Charles Itembe

Muktasari:

  • Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe alisema licha ya mikopo inayotolewa kwa mwanachama kwa udhamini wa mwajiri, pia itatolewa kwa vyama vya akiba na mikopo (Saccos).

Arusha. Benki ya Azania kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), itaanza kutoa mikopo kwa wanachama wa mfuko huo ili kuboresha maisha na kuhamasisha matumizi ya huduma fedha nchini.

Mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Charles Itembe alisema licha ya mikopo inayotolewa kwa mwanachama kwa udhamini wa mwajiri, pia itatolewa kwa vyama vya akiba na mikopo (Saccos).

“Tumetenga Sh50 bilioni kuzikopesha Saccos zilizopo na zitakazoanzishwa maeneo ya kazi,” alisema Itembe.

Licha ya Saccos zilizopo maeneo ya kazi, Itembe alisema ipo programu inayozihusisha za hiari ambayo itamwezesha mwanachama kupata mkopo hadi wa Sh20 milioni.

“Huu ni mpango wa majaribio iwapo utafanikiwa tutaupa kipaumbele,” alisema.

Benki hiyo inamilikiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa asilimia 98. Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki (EADB) kwa asilimia 1.5 na wanahisa wengine 48 wakimiliki asilimia moja.

Mpaka Juni mwaka jana, mifuko hiyo ilikuwa na jumla ya wanachama milioni 2.23 ambao michango yao ilikuwa Sh2.15 trilioni huku wastaafu 126,358.

Naye Meneja mwandamizi wa huduma za rejareja wa Azania, Jacskon Lohay aliwataka Watanzania na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii kuchangamkia mikopo hiyo na huduma nyingine wanazotoa.