Balozi akumbusha kazi za fasihi

       Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak      

Muktasari:

Malika alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye tamasha la fasihi lililofanyika nyumbani kwake na kuwakutanisha Watanzania na Wafaransa wanaoishi nchini.

       Dar es Salaam. Balozi wa Ufaransa nchini, Malika Berak amesema mipango ya kujenga uchumi imara iende sambamba na kuimarisha diplomasia ya utamaduni baina ya Tanzania na mataifa mengine.

Malika alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye tamasha la fasihi lililofanyika nyumbani kwake na kuwakutanisha Watanzania na Wafaransa wanaoishi nchini.

“Tunapozungumzia maendeleo ya sekta za mafuta na gesi au utalii na miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi tusisahau uhusiano wa jamii. Kujikita huko tunafanya mambo mengine yasahaulike, utamaduni ni muhimu kama yalivyo maendeleo ya uchumi,” alisema.

Naye mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mkuki na Nyota, Walter Bugoya alisema waandishi wengi wanapenda kuandika Kiingereza ambacho kina wasomaji wachache nchini hivyo kujipunguzia soko.

Licha ya hiyo, Bugoya alisema Watanzania wengi hawana utamaduni wa kusoma vitabu ukiacha uwezo mdogo wa kuvinunua.

“Nashauri Serikali ingewekeza kwa waandishi wa vitabu kama inavyofanya kwa wataalamu wa fani mbalimbali,” alisema Bugoya.