Bodaboda walivyowakimbiza wachoma mkaa Mkuranga

Muktasari:

  • Kati ya wavunaji saba wa misitu wenye leseni, sita wamezirudisha

Wavunaji wakubwa wa mazao ya misitu na wauzaji wa mkaa wilayani hapa, wamelazimika kurudisha leseni zao kwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) baada ya kushindwa kuhimili ushindani wa soko.

Meneja wa TFS Wilaya ya Mkuranga, Christina Mohamed alisema wadau hao wamesitisha uvunaji kutokana na kuongezeka kwa madereva wasafirishao mkaa kwa pikipiki ambao huingia vijijini kinyemela na kuununua kwa Sh20,000 badala ya Sh12,000 wanayolipa wao kila kiroba.

Inadaiwa kwa siku takriban vijana 30 huomba leseni za usafirishaji mkaa kutoka ofisi za TFS Mkuranga kwenda jijini Dar es Salaam, idadi inayokadiriwa kuwa maradufu ya wanaoingia kinyemela kufuata huduma hiyo.

“Hivi sasa bodaboda wasafirishao mkaa wameongezeka zaidi na wengi wanaingia vijijini kinyemela. Hali hii imesabisha wavunaji wakubwa wanaolipia leseni na vitu vyote kisheria kushindwa kuhimili ushindani wa soko,” alisema Christina.

Alisema kinachowaumiza wavunaji hao, hupaswa kununua kiroba kimoja kwa Sh12,000 kwa sababu wameshalipia gharama zote za kisheria TFS lakini bodaboda wananunua Sh20,000 kinyemela.

Kutokana na hali hiyo, Christina alisema wavunaji hao wenye leseni hushindwa kupata bidhaa na wakitaka kununua kwa Sh20,000 wanapata hasara.

Christina alisema wakala huo unashindwa kufanya doria kuwadhibiti bodaboda hao kwa kuwa ofisi hiyo haina gari, kwa sasa wanatumia gari moja na Wilaya ya Rufiji.

Ofisa maduhuli na takwimu wa TFS Mkuranga, Andrew Chibwana alisema bodaboda wameongezeka mwaka huu baada ya kuruhusu usafirishaji mkaa kwa pikipiki na kila siku ofisi hiyo hupokea vijana 30 au zaidi wanaochukua vibali kupeleka mkaa Dar es Salaam.

Alisema kila kibali hulipiwa Sh40,000 hivyo ofisi hiyo kuingiza wastani wa Sh1.2 milioni kwa siku, lakini ongezeko la wasio na vibali linatishia mapato hayo.

“Inabidi itafutwe mbinu ya kudhibiti ongezeko la vijana hawa kutoathiri mapato ya Serikali,” alisema Chibwana.

Kutokana na ukwepaji wa tozo za usafirishaji wa maliasili za misitu, inaelezwa Serikali hupoteza wastani wa Sh80 milioni wilayani humo kwa mwaka.