Brela yaagiza wenye kampuni kuhakiki taarifa mtandaoni

Muktasari:

  • Awali, endapo taarifa za wakurugenzi na wanahisa wa kampuni zikiwa haziendani na zile za Brela walikuwa wanapaswa kusafiri hadi Dar es Salaam kupata baadhi ya huduma ambazo kwa sasa zinapatikana mtandaoni ndani ya nusu saa badala ya siku saba za mwanzo.

Dar es Salaam. Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), imewaagiza wafanyabiashara waliosajili kampuni kabla ya Februari mosi, 2018 kuhakiki taarifa ili ziingie katika mfumo unaotaka kusajiliwa kwa mtandao.

Awali, endapo taarifa za wakurugenzi na wanahisa wa kampuni zikiwa haziendani na zile za Brela walikuwa wanapaswa kusafiri hadi Dar es Salaam kupata baadhi ya huduma ambazo kwa sasa zinapatikana mtandaoni ndani ya nusu saa badala ya siku saba za mwanzo.

Ofisa mtendaji mkuu na msajili wa kampuni wa Brela, Frank Kanyusi alisema jana kuwa, uhakiki wa taarifa ni muhimu kwa kuwa unampunguzia mwenye kampuni muda wa kuzunguka.

“Uhakiki huo haumlazimu mfanyabiashara kwenda Brela kwani atapaswa kuhakiki hapohapo alipo kwa njia ya mtandao. Maboresho ndani ya taasisi yanamwezesha kila Mtanzania au mfanyabiashara kunufaika na huduma zetu,” alisema Kanyusi.

Akifafanua, alisema wamiliki wa ndani ya nchi watahitajika kuweka namba ya mlipa kodi (Tin) na namba za kitambulisho cha taifa ambapo taarifa zote zitapatikana, huku kampuni zinazomilikiwa na raia wa kigeni wakurugenzi watatakiwa kuweka namba ya mlipa kodi na pasi za kusafiria.

Kanyusi alisisitiza kuwa ifikapo mwishoni mwa Aprili, mwaka huu, ofisi yake itazindua mfumo mpya sambamba na utoaji leseni daraja A na B ambapo ile ya daraja A inatolewa na Brela na B itatolewa na ofisi za halmashauri.

“Atapata usajili wa kampuni, TIN na leseni ndani ya saa nne, hivyo leo (jana) kampuni zilizosajiliwa kabla ya Februari mosi 2018 wahakiki taarifa zao kwa kuzingatia mfumo huu mpya ili nazo ziwe katika mfumo, kwa sababu awali uwasilishaji taarifa haukua sahihi,” alisema na kuongeza:

“Hivyo tunataka wao watuletee taarifa wanazoona ndizo sahihi na tulinganishe na tulizonazo kisha tunakubaliana zipi ni sahihi.”

Alisema taarifa ziingizwe kwenye mtandao badala ya mtu kusafiri hadi Dar es Salaam kuziwasilisha.

Mkuu wa kitengo cha kampuni kutoka Brela, Rehema Kitambi alisema wametenga chumba maalumu ofisini kwao kwa ajili ya kuwasikiliza wateja wanaotaka kujisajili kwa njia ya mtandao.

“Hivyo (wateja) waje tutawahudumia na kila swali litapata jibu, naamini wakishazoea kila kitu kitakwenda sawa na ufanisi utaongezeka,” alisema.