DC aapa kula sahani moja na wahujumu

Muktasari:

Korosho hizo zipatazo tani 8,300 zilizokataliwa kupokelewa katika vyama vikuu, zinadaiwa kupokewa kwa wingi Januari zikiwa hazina ubora hali inayochafua soko la korosho za wilayani humo.

Newala. Baada ya baadhi ya vyama vya msingi (Amcos) wilayani Newala mkoani Mtwara kudaiwa kupokea korosho zisizokuwa na ubora kutoka nje ya mkoa, uongozi wa wilaya hiyo umesema utaunda tume kuchunguza tuhuma hizo.

Korosho hizo zipatazo tani 8,300 zilizokataliwa kupokelewa katika vyama vikuu, zinadaiwa kupokewa kwa wingi Januari zikiwa hazina ubora hali inayochafua soko la korosho za wilayani humo.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa korosho juzi, mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo alisema hali hiyo haivumiliki kwa kuwa inahatarisha soko la zao hilo kwa wilaya hiyo na mkoa.

“Korosho zilizokataliwa mwakani hazitaingia kwenye mzunguko wa soko, hivyo kushusha soko la Mtwara kwa sababu ni nyingi ambazo vyama vya msingi kama havitakagua vizuri kabla ya kupeleka ghala kuu naiona hatari hiyo,” alisema Mangosongo na kuongeza:

“Binafsi nimeshtuka kuambiwa zimepelekwa tani 8,300 ndani ya wiki mbili, vilevile ili tutende haki tutaunda tume ambayo itapita kwa kila chama kuangalia hizo korosho zenu.”

Akizungumzia suala hilo, meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (Tanecu), Mohamed Nassoro alisema ongezeko hilo la korosho linaleta wasiwasi kwa sababu mnada wa Desemba 2017 ulikuwa na tani 600, lakini Januari 2018 zimeongezeka na kufikia tani 8,300 licha ya wakulima kuwa wachache.

“Desemba na kuendelea mara nyingi uzalishaji korosho na makusanyo hupungua katika maghala makuu ya minada, lakini tulipokwenda mnada wa tisa Desemba tulikuwa na tani 600 wiki mbili baadaye makusanyo katika maghala yote kulikuwa na tani 8,300,” alisema Nassoro na kuongeza:

“Hii kidogo imetupa wasiwasi, inawezekana huenda kuna makusanyo ya korosho kutoka vyanzo ambavyo si rasmi au si katika mashamba ya wakulima wetu tunaowajua.”

Wakati minada ikielekea mwishoni baadhi ya wanunuzi wamegoma kulipia korosho kwa madai kuwa hazina ubora.

Ukusanyaji korosho

Mwenyekiti wa Amcos, Ismail Chilomba alisema uuzaji korosho msimu unapoanza makusanyo yake yanakuwa madogo lakini huongezeka sambamba na makusanyo kadri zinavyokomaa.

“Ukusanyaji wa korosho kulingana na maeneo yetu, msimu unapoanza Septemba hadi Oktoba uuzaji unakuwa kidogo ukilinganisha na Novemba hadi Januari, kwa hiyo makusanyo ya mwanzoni yatakuwa machache kwa sababu uwanda wetu mkubwa unazaa korosho kipindi cha masika, lazima uangaliwe ndiyo unaozidisha tani hizo,” alisema Chilomba.

Bei ya msimu huu

Korosho ghafi msimu wa mwaka 2017/18, bei ya juu ni Sh4,128 kwa kilo na bei ya chini ni Sh2,300.

Ufufuaji korosho

Februari mwaka jana Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ilianza mpango wa kugawa bure miche ya zao hilo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji.

Profesa Peter Masawe ambaye ni mtafiti gwiji wa kimataifa wa korosho, anasema Tanzania inasimama katika nafasi nzuri ya kuongeza uzalishaji korosho ambalo ndilo zao lililobaki pekee lenye mipango endelevu na lenye soko lisiloyumba kwa sasa.

Mkakati huo utakuwa ni endelevu na utakuwa kichocheo cha kupanda mikorosho mipya.