Dangote kulima mpunga na wasomi wa vyuo vikuu

Muktasari:

  • Mpango huo unaotekelezwa na kampuni yake ya Dangote Rice Limited iliyojikita kwenye kilimo hicho,katika Jiji la Kogi nchini Nigeria, unalenga kupunguza uhaba wa ajira kwa wahitimu hao.

 Katika kuongeza uhakika wa chakula na ajira kwa vijana, bilionea namba moja Afrika, Aliko Dangote ameanzisha mpango wa kuwashirikisha wahitimu wa vyuo vikuu kulima mpunga.

Mpango huo unaotekelezwa na kampuni yake ya Dangote Rice Limited iliyojikita kwenye kilimo hicho,katika Jiji la Kogi nchini Nigeria, unalenga kupunguza uhaba wa ajira kwa wahitimu hao.

Katika utekelezaji huo kampuni hiyo inawashirikisha wahitimu hao kulima hekta 100 kwa ahadi ya kununua mpunga utakaozalishwa huku yenyewe ikitoa mbegu, ushauri wa namna ya kukabiliana na changamoto za kilimo, viuatilifu na mbolea.

Mkurugenzi Mtendaji wa Dangote Rice, Devakumar Edwin alisema mradi huo ni sehemu ya kuwaandaa wajasiriamali watakaoleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa sekta hiyo.

“Tunaamini ujuzi, maarifa, mazingira rafiki na ushirikiano katika mnyororo wa thamani ni miongoni mwa mambo yatakayofanikisha mapinduzi ya kilimo. Mradi huu utatatua changamoto ya maarifa yanayohitajika katika uzalishaji wa mpunga miongoni mwa vijana,” alisema Edwin.

Mpango huo unakusudia kupunguza ombwe la uzalishaji na mahitaji ya mpunga nchini humo pamoja na kuongeza ufanisi wa mashine nyingi za kukoboa ambazo zinafanya kazi chini ya asilimia 20 kutokana na ubora usiokidhi viwango vya mpunga unaozalishwa.

Takwimu za Wizara ya Kilimo nchini humo zinaonyesha mpaka mwaka 2015, mahitaji ya mchele yalikuwa tani za ujazo milioni 6.3 huku uwezo wa kuzalisha ukiwa tani milioni 2.3.

Mkurugenzi huyo aliwataka vijana hao kujikita kwenye kilimo hicho ili kukuza kipato na ustawi wa familia zao. Mradi una zaidi ya hekta 25,000 za wakulima wadogo na mpaka mwakani, unatarajiwa kuanza kuzalisha tani milioni moja za ujazo.

Mchumi na mkurugenzi wa shahada za juu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema kinachofanywa na Dangote kinapaswa kuigwa na nchi nyingine.

“Tunatoa ruzuku kwa wakulima lakini hakuna miundombinu iliyo tayari kufanikisha kilimo. Sera zetu ni za jumla suala linalochelewesha kuyaona matunda ndani ya muda mfupi,” alisema Dk Pastory.