Dk Kigwangalla: Miezi sita hakuna ujangili uliotokea

Muktasari:

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alipozungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini hapa.

Dodoma. Serikali imesema imefanikiwa kudhibiti ujangili kwa zaidi ya asilimia 50 na nyara zinazokamatwa hivi sasa ni masalia ya zamani.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alipozungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke ofisini kwake mjini hapa.

Mazungumzo hayo yalilenga kujadili mambo mbalimbali ikiwamo kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili katika uhifadhi na maendeleo ya utalii.

“Katika miezi sita iliyopita hakuna mauaji mapya ya wanyamapori yaliyoripotiwa. Nyara zinazokamatwa hivi sasa yakiwamo meno ya tembo na ngozi za wanyama, ni masalia ya zamani,” alisema Dk Kigwangalla.

Mafanikio hayo alisema yalitokana na juhudi zinazofanywa kudhibiti ujangili zikiwamo doria za mara kwa mara zinazoshirikisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama raia wema.

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi maeneo ya hifadhi na kuanzisha jeshi maalumu la usimamizi wa misitu na wanyamapori, kuifanyia marekebisho sheria ya wanyamapori na taasisi za uhifadhi.

Vilevile, Dk Kigwangalla alimueleza Balozi Cooke kuwa Serikali inaimarisha vivutio vya utalii kwa kupanua jiografia ya maeneo na kuongeza vivutio.

Katika kuongeza vivutio, alisema Serikali itajenga makumbusho ya marais wastaafu wa Tanzania mjini Dodoma na kuanzisha makumbusho ya meno ya tembo Dar es Salaam, Arusha, Iringa na Dodoma.

Sambamba na hayo, kila Septemba utakuwa mwezi maalumu wa maadhimisho ya urithi wa Mtanzania pamoja na kuanzisha mamlaka ya usimamizi na uendelezaji, kuimarisha utalii wa fukwe na kuitambua barabara iliyotumika katika biashara ya utumwa.

Balozi Cooke alisema Uingereza itaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya, rushwa na ujangili.

“Zaidi ya watalii 75,000 wa Uingereza hutembelea Tanzania kila mwaka na wengine wamewekeza katika sekta hiyo nchini. Naiomba Serikali irekebishe baadhi ya changamoto zilizopo katika sekta hiyo hasa mtiririko wa kodi,” alisema Cooke.

Balozi Cooke alisema mtiririko wa kodi unakwaza utalii na uwekezaji katika sekta h iyo, hivyo unahitaji marekebisho kuhakikisha mapato ya taifa yanaongezeka kama zilivyo sekta nyingine. Aliahidi kuendelea kusaidia kuboresha sekta hiyo.