H’shauri yatenga Sh19 mil kununua miche ya kahawa

Muktasari:

Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo, Chikira Mcharo alisema fedha hizo zitasaidia kununua miche zaidi ya 63,000 aina ya vikonyo.

Moshi. Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro imetenga Sh19 milioni kwa ajili ya kununua miche ya kahawa kwa kipindi cha mwaka 2017/18 katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).

Ofisa kilimo wa halmashauri hiyo, Chikira Mcharo alisema fedha hizo zitasaidia kununua miche zaidi ya 63,000 aina ya vikonyo.

“Mwaka 2016/17 tulitenga Sh15.5 milioni na tulinunua miche 42,000,” alisema Mcharo.

Alifafanua kuwa kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 Sh7.5 milioni zilitengwa kwa ajili ya kukarabati vituo vya kuuzia kahawa.

“Pia, tumeweza kukarabati mifereji ya maji 49 kati ya 200 iliyopo kwa kipindi cha mwaka 2014/17,” alisema.

Mratibu wa zao hilo katika halmashauri hiyo, Violeth Kisanga aliwataka wakulima wa zao hilo kuachana na kilimo cha zamani cha kahawa aina ya KP 423 na badala yake walime kahawa ya vikonyo kutoka TaCRI.

“Kahawa ya zamani inashambuliwa sana na magonjwa, ila hii ya vikonyo haishambuliwi sana na huzaa kwa wingi, huu ni wakati wa mkulima kubadilika ili anufaike na shamba na kahawa basi alime kahawa ya vikonyo,” alisema Kisanga.

Kuhusu mbolea ya DAP, Kisanga alisema baada ya Serikali kuona gharama ya uuzwaji wake ipo juu iliziagiza mamlaka husika kushusha bei.

Alisema tangu mwaka 2016/2017 mbolea hiyo imekuwa ikiuzwa kwa Sh51,924 kwa mfuko wa kilo 50 badala ya Sh70,000 ya awali.

Wajumbe wa Bodi ya Muungano wa Vyama vya Ushirika Uru Kaskazini ambao pia ni wakulima wa zao hilo, Felix Masao na Proti Mauki waliiomba halmashauri kuwasaidia wakulima pembejeo ikiwamo dawa kwa bei nafuu.