January awapa darasa la ajira vijana wa Mzumbe

Muktasari:

  • Alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kongamano la kubadilisha fikra kwa vijana wasomi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe lililoandaliwa na jukwaa la vijana kwa ajili ya kutambua fursa, mitaji na masoko.

Morogoro. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amewataka vijana wasomi kuacha kuwaza ajira serikalini na kampuni kubwa, badala yake watafute fursa katika kilimo, viwanda na biashara ili wajiajiri.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kongamano la kubadilisha fikra kwa vijana wasomi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe lililoandaliwa na jukwaa la vijana kwa ajili ya kutambua fursa, mitaji na masoko.

Alisema Serikali haiwezi kuajiri wasomi wanaohitimu vyuo, hivyo katika kuelekea uchumi wa viwanda wana fursa ya kufanya shughuli za kujipatia kipato.

Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba alisema wakati huu wa ulimwengu wa sayansi na teknolojia lazima vijana wabadilishe fikra za kusubiri kuajiriwa na watafute maarifa ya kujiajiri.

Ruge alisema katika kuelekea uchumi wa viwanda vijana wana nafasi ya kupiga hatua ya maendeleo kupitia sekta ya viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na shughuli nyingine za ujasiliamali.