Kampuni mbili za umeme Tanzania zang’ara tuzo kimataifa Italia

Muktasari:

  • Mkurugenzi mtendaji wa Ensol, Khamis Mikate na mkurugenzi mwenza wa RVE, Franz Kottulisnky walisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, kampuni zao zilipata tuzo na kuiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa la uwekezaji wa umeme vijijini liitwalo Alliance for Rural Electrification (ARE) Investment Forum.

Dar es Salaam. Kampuni za Ensol Tanzania na Rift Valley Energy (RVE), zimepata tuzo za kimataifa nchini Italia kutokana na ufanisi katika miradi ya umeme inayotekelezwa vijijini.

Mkurugenzi mtendaji wa Ensol, Khamis Mikate na mkurugenzi mwenza wa RVE, Franz Kottulisnky walisema jijini Dar es Salaam jana kuwa, kampuni zao zilipata tuzo na kuiwakilisha vyema Tanzania katika jukwaa la uwekezaji wa umeme vijijini liitwalo Alliance for Rural Electrification (ARE) Investment Forum.

Jukwaa hilo liliwashirikisha wawakilishi wa kampuni na taasisi kutoka Afrika, Asia, Amerika na Ulaya ambapo lilifanyika katika Kisiwa cha Sicily kuanzia Machi 13 hadi 17.

Mikate alisema katika jukwaa hilo kampuni zilitambuliwa kwa kuendeleza mpango wa umeme vijijini kwenye nchi zao na kujikita katika mawazo endelevu. Naye Kottulisnky alisema, “Kati ya makundi saba, miradi miwili ya umeme vijijini nchini Tanzania ilichaguliwa kuwa washindi wa tuzo ya ARE ya 2018 kwenye makundi tofauti.”

Katika kundi la nne la sekta binafsi kwenye nchi zinazoendelea, RVE ilipata tuzo kutokana na ubunifu wake kupitia mradi wa Mwenga Hydro ulioiwezesha kuzalisha umeme wa maji wa megawati nne na kuunganishwa katika gridi ya Taifa sambamba na kuusambaza katika mtandao wa kilomita 300 zilizopo eneo ya Mufindi na Kihansi unaoziwezesha nyumba 3,000 kupata nishati hiyo.

Mikate alisema kwenye kundi la sita la miradi bora ya umeme vijijini, Ensol ilinyakua tuzo kupitia mradi wake wa Kijiji cha Mpale kilichopo kwenye Milima ya Usambara wilayani Korogwe unaotoa na kusambaza umeme wa kilowati 48 kutokana na mionzi ya jua ambao unahudumia nyumba 250 zenye wakazi wapatao 3,000.