Kampuni ya bia yawajaza wawekezaji wake DSE

Muktasari:

  • Licha ya kupanda kwa hisa za TBL, mauzo ya DSE yamepanda kutoka Sh1.5 bilioni wiki iliyoishia Oktoba 6 hadi Sh30 bilioni ilipofika Oktoba 13 na hisa zilizouzwa zikiongezeka kutoka 600,000 hadi milioni 2.5.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imeongoza mauzo katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na kuwapa faida ya kati ya asilimia 2.3 mpaka 7.7 waliofanya miamala hiyo kwa wiki iliyoisha Oktoba 13.

Licha ya kupanda kwa hisa za TBL, mauzo ya DSE yamepanda kutoka Sh1.5 bilioni wiki iliyoishia Oktoba 6 hadi Sh30 bilioni ilipofika Oktoba 13 na hisa zilizouzwa zikiongezeka kutoka 600,000 hadi milioni 2.5.

TBL iliongoza mauzo hayo kwa asilimia 99.6 ikifuatiwa na Benki ya CRDB kwa asilimia 0.2 na Vodacom asilimia 0.1.

Kampuni hiyo ilifanikiwa kuuza hisa milioni 2.1, kati ya hizo 736,259 ziliuzwa kwa Sh13,900 kila moja na 1,348,235 kwa Sh14,000.

Taarifa ya wiki ya soko hilo inasema mwanzoni, Oktoba 9, hisa za TBL zilikuwa zinauzwa Sh13,000 lakini mpaka Oktoba 13 zilifikia Sh13,500 kwa bei za kawaida wakati waliouziana moja kwa moja ilikuwa kati ya Sh13,900 hadi Sh14,000.

Meneja mkuu wa kampuni ya Orbit Securities, Simon Juventus alisema TBL inakimbiliwa kwa sababu imetangaza gawio la Sh470 kwa kila hisa kwenye awamu ya pili baada ya kutangaza Sh100 katika awamu ya kwanza.

“Gawio walilotangaza limewavutia wawekezaji wengi ndiyo maana hata bei ya hisa imeongezeka. Watu wanazikimbilia ili kupata gawio hilo,” alisema Juventus.

Alisema kampuni inayofanya vizuri sokoni huvuta macho ya wawekezaji wengi hasa kunapokuwa na mambo yanayotarajiwa kama ilivyo kwa gawio.

Licha ya mwenendo huo, ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa sokoni hapo umeshuka kwa Sh362 bilioni kutoka Sh20.8 trilioni hadi Sh20.4 trilioni wiki iliyoishia Oktoba 13.

Sababu za kupungua kwa mtaji huo zimeelezwa kuwa ni kushuka kwa bei ya hisa za Benki ya KCB kutoka Sh950 hadi Sh820, kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL) kutoka Sh5,460 hadi Sh5,420 na zile za NMG kutoka Sh2,390 hadi Sh2,380.

Aidha, kutokana na kupanda bei ya hisa za TBL kwa asilimia 0.75, ukubwa wa mtaji wa kampuni za ndani umeongezeka kwa Sh29 milioni kutoka Sh9.93 trilioni kwa wiki iliyoishia Oktoba 6 hadi Sh9.96 trilioni wiki ya Oktoba 13.

Mauzo ya hati fungani yaliongezeka pia kutoka Sh2.18 bilioni mpaka Sh9 bilioni ndani ya muda huo.