Kutuma fedha airtel money bure kuanzia laki mbili

Muktasari:

Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando amesema kuanzia sasa wateja wa Airtel Money wanaweza kutuma pesa bila tozo yoyote iwapo atatuma kuanzia kiasi cha Sh200,000 au zaidi.

 Kama ni mteja wa simu za mkononi na unaogopa kutumia huduma za kifedha kutokana na gharama, basi kampuni ya Airtel wamekufikiria. Kampuni hiyo imeanzisha utaratibu mpya ambao mtu ambaye anatuma fedha kuanzia Sh200,000 na zaidi hatotozwa ada yoyote.

Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando amesema kuanzia sasa wateja wa Airtel Money wanaweza kutuma pesa bila tozo yoyote iwapo atatuma kuanzia kiasi cha Sh200,000 au zaidi.

“Huduma hii ni kwa wale wanaotuma kwenda mtandao wowote ule, iwe Airtel kwa Airtel au kutoka Airtel kwenda mitandao mingine,” amefafanua Mmbando.

Mmbando amesema kampuni hiyo inalenga kutimiza ahadi wanazozitoa kupitia kauli mbiu zao.

“Airtel Money bado tunawaambia wateja wetu relax (tulia)… huduma hii itakuwa na tija sana kwa wafanyabiashara au wateja wote wanaotaka kulipana pesa kuanzia kiwango cha Sh200,000 na kuendelea kwa kuwa wataokoa pesa nyingi sana watakazoweza kuzitumia kwa matumizi mengine,” anafafanua na kuongeza:

“Airtel Money tunaondoa tozo hizo kwa wateja wetu ili kuongeza ulinzi kwa kuwajengea wateja utaratibu wakutobeba pesa nyingi kwa wakati mmoja hivyo kuimarisha swala la usalama wa pesa zao kwa kuwa akaunti ya Airtel Money ni salama muda wote.”

Mmbando alifafanua kuwa wateja wanaotuma pesa chini ya kiasi hicho wataendelea kutozwa ada ingawa kiwango cha ada hizo ni kidogo sana ukilinganisha na kampuni nyingine.