Mahindi yaliyooza sumu kwa mifugo

Muktasari:

Ushauri huo ulitolewa juzi na ofisa mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Daniel Moshy wakati akifunga kongamano la udhibiti wa sumu kavu lililofanyika kwa siku mbili likishirikisha Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Umoja wa Udhibiti Sumu Kuvu Afrika (Paca)

       Dar es Salaam. Katika kuhakikisha Taifa linaondokana na tatizo la sumu kuvu, wakulima na wafugaji wametakiwa kuacha kuipa mifugo mahindi yaliyooza.

Ushauri huo ulitolewa juzi na ofisa mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Daniel Moshy wakati akifunga kongamano la udhibiti wa sumu kavu lililofanyika kwa siku mbili likishirikisha Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Umoja wa Udhibiti Sumu Kuvu Afrika (Paca)

Alisema mahindi mengi yaliyooza yameathiriwa na sumu kuvu, hivyo husababisha baadhi ya mifugo kudumaa katika hatua ya ukuaji kutokana na ulaji wa nafaka hizo. “Mara nyingi tumekuwa tukiendelea na suala la upigaji marufuku matumizi ya mahindi yaliyooza kwa wanyama kama vile nguruwe pamoja na kuku ili kuisaidia mifugo hiyo isiathirike,” alisema Moshy.

Ofisa huyo aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa, wakati mwingine kuku hupata ugonjwa unaosababishwa na sumu kuvu, lakini chanzo chake ni wafugaji kuwapatia mahindi yaliyooza.

Alisema wafugaji wanatakiwa kuepuka kuwapa wanyama mahindi hayo kwa kuwatafutia yaliyo salama ambayo hayajaingiliwa na fangasi wanaosababisha sumu hiyo. Mkurugenzi mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo alisema katika kongamano hilo wamekubaliana kupambana kwa kadri ya uwezo wao ili kuondokana na sumu hiyo hasa kwa nchi za Afrika, ambapo imeonekana kushamiri kwa muda mrefu.

Alisema mojawapo wa hatua waliyofikia katika umoja huo ni kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wafugaji kutoa elimu juu ya tatizo hilo.

“Wapo wafanyabiashara wanashindwa kupata masoko, hivyo TFDA itaendekea kutoa elimu tangu mazao hayo yanapofikia hatua ya uvunaji,” alisema Sillo.

Kwa upande wake, mshauri kutoka Paca, Martn Kimanya alisema pamoja na kutoa elimu kwa wananchi lakini wafanyabiashara wanatakiwa kuweka utaratibu mzuri wa kuhifadhi mazao hayo na pia pindi yawapo shambani.

Alisema sumu kuvu inaleta madhara makubwa kwa binadamu na wanyama na hivyo lazima kuwapo na uangalizi wa kutosha.