Mchele wa Tanzania wasifiwa nje ya nchi

Muktasari:

  • Watalaamu wa nje wawapongeza wanawake

Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha mchele bora ambao una thamani ikilinganishwa na ule unaozalishwa Msumbiji, Kenya, Rwanda na Burundi.

Sambamba na hilo, pia imetajwa kuwa nchi yenye idadi kubwa ya wanawake wanaozalisha kwa wingi zao hilo ambao hulima kati ya tani tano hadi nane kwa eka tofauti na Msumbiji na Kenya.

Mtaalamu wa kilimo kutoka Jimbo la Zambezia nchini Msumbiji, Jaime Gado alisema juzi alipotembelea nchini akiwa na wataalamu wa mpunga saba na mmoja kutoka Japan kwa lengo la kubadilishana ujuzi na kujifunza kutoka kwa wakulima wa Tanzania.

Gado alisema mbali na changamoto ya kuwa na mashine zilizochakaa na ubovu wa miundombinu ikiwemo barabara, mkulima wa Tanzania ana ari ya kuzalisha mpunga bora. “Tumeona changamoto kadha wa kadha, lakini bado mkulima huyu amekuwa akizalisha kilicho bora, tatizo ni uhakika wa soko, nashauri mamlaka husika kuangalia namna ya kumsaidia mkulima huyu ili pia aweze kuuza kwa wingi katika nchi zinazozunguka Bara la Afrika,” alisema.

“Pia nawapongeza Jica kwa kuweka utaratibu wa kuongeza thamani ya zao hili kwa kusaidia kusimamia makubaliano kati ya wanunuzi na wakulima kwa wakulima wa Tanzania kwani imekuwa mkombozi kwa wakulima wengi hususan waliopo kwenye skimu ya Lower Moshi.”

Akizungumza wakati wa mafunzo ambayo yalilenga kubadilishana uzoefu na wataalamu wa kilimo nchini, mshauri mkuu wa ufundi katika mradi wa maendeleo ya uzalishaji wa mpunga, Monitori Tomitaka alisema idadi kubwa ya wazalishaji ni wanawake

Mshauri huyo wa mradi huo ambao unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (Jica), alisema mwaka 2014 Tanzania ilizalisha tani 925 kwa hekta.

“Kwa Tanzania eneo linalolima mpunga ni kilomita za mraba 945,087 niwashauri wakulima kuzingatia makubaliano wanayokubaliana na wanunuzi wa mpunga ili wanaozalisha uzidi kuwa na thamani,” alisema Tomitaka.

Mtaalamu kutoka Tanzania, Shedrack Msemo alitaja changamoto wanazokumbana nazo wakulima kuwa ni pamoja na miundombinu mibovu ya kuingia kwenye mashamba, kutokuwa na mashine bora za ukoboaji wa mpunga pamoja na za kuvunia.

Jica inatekeleza mradi wa Tanrice 2 nchini Tanzania na Proapa nchini Msumbiji na wataalamu wamekuwa wakibadilishana ujuzi kwa lengo la kusaidia kuongeza uzalishaji.