Mgodi unavyoikosesha mapato halmashauri

Muktasari:

        Madiwani wadai hawana majibu kwa wananchi walioambiwa kuomba kazi

Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wamehoji sababu za kusimama kufanya kazi Mgodi wa Dhahabu Magambazi.

Wakizungumza kwenye mkutano maalumu cha baraza la madiwani kujadili rasimu ya mapendekezo ya mpango wa bajeti yao ya mwaka 2018/19 juzi, madiwani hao walisema walipewa taarifa kuwa kazi zingeanza Oktoba mwaka jana ila mpaka sasa hakuna kinachoendelea na halmashauri inakosa mapato.

Diwani wa Segera, Yasini Mtamike alisema wanashindwa kufahamu sababu za wawekezaji waliopo eneo hilo kutoanza kazi, bila taarifa rasmi.

Mtambike alisema maswali yamekuwa ni mengi kwao kutoka kwa wananchi wakihoji sababu za mgodi kukaa kimya, ilhali waliambiwa waandike barua kuomba kazi mbalimbali.

“Tunashindwa kujibu maswali kutoka kwa wananchi wetu, lakini hali hiyo pia inasababisha halmashauri kukosa mapato hivyo ni vizuri tupewe taarifa juu ya suala hili,” alisema.

Akitolea ufafanuzi wa suala hilo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Handeni, William Makufwe alisema wamebaini kuna tatizo kwa wawekezaji wa machimbo hayo kwa kuwa hawajaweka makubaliano yao sawa.

Makufwe alisema tayari kuna hatua za kisheria wamechukua kuhusu ukimya wa Magambazi kutokana na kuathiri mapato ya halmashauri, kwa miaka miwili imepata hasara ya Sh500 milioni na makadirio ya kila mwezi walitakiwa kulipa Sh25 milioni.

Bajeti yapita

Baraza hilo kwa kauli moja, limepitisha rasimu ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/19 ikiwa ni zaidi ya Sh49 bilioni kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Bajeti hiyo ina ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na ya mwaka huu wa fedha 2017/18, ambayo ilikuwa zaidi ya Sh38 bilioni.

Akiwasilisha mapendekezo hayo, ofisa mipango wa halmashauri hiyo, Edina Kataraiya alisema bajeti inajumuisha mishahara, matumizi mengineyo ya miradi, utoaji huduma za jamii, uongozi na usimamizi.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Handeni, Ramadhani Diliwa alisema bajeti hiyo itangalia zaidi mapato ya ndani siyo kutoka Serikali Kuu kwani fedha hizo zimekuwa zikichelewa kufika na kusababisha baadhi ya miradi usimama.