Miradi ya Tasaf yaajiri Wahadzabe

Maji nio miongoni mwa huduma zitakazopatikana baada ya miradi kukamilika.

Muktasari:

Miradi hiyo yenye thamani Sh562 milioni imeanzishwa na mpango wa kunusuru kaya masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa ajili ya kabila hilo.

Mkalama. Watu wa kabila la Wahadzabe wanaoishi Kijiji cha Kipamba, Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, wanatarajia kupata ajira za muda katika miradi ya ujenzi itakayoanzishwa eneo hilo.

Miradi hiyo yenye thamani Sh562 milioni imeanzishwa na mpango wa kunusuru kaya masikini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwa ajili ya kabila hilo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji juzi, Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida, Patrick Kasango alisema Sh562.7 milioni zimenunulia vifaa vinavyotumika kwenye miradi hiyo inayotoa fursa za ajira za muda kwa walengwa.

“Ajira hizi za muda zimelenga kuziongezea kipato kaya zilizoandikishwa kwenye mpango wa Tasaf III. Pia, wakati huohuo zitakuwa zimeshiriki kuondoa kero zinazowakabili katika maeneo yao, ikiwamo uhaba wa maji, zahanati na barabara,” alisema Kasango.

Kasango alisema licha ya mafanikio hayo, wanakabiliwa matatizo mbalimbali ikiwamo uhaba wa magari, barabara mbovu ambazo wakati wa masika hazipitiki na baadhi ya kaya kutembea umbali mrefu kwenda kituo cha uhaulishaji fedha na maeneo kutokuwa na huduma za simu.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Edward Mkumbo licha ya kuipongeza Serikali na wadau kwa kushirikisha Wahadzabe kwenye mpango wa Tasaf, wanaomba kuwajengea barabara.

“Kama mpango huu usingeanzishwa kwetu, hali ingekuwa mbaya kwa sababu vyakula vyetu vya asili havipatikani tena. Kama mnavyojua hatuna utamaduni wa kulima, niiombe Serikali itupatie wahudumu wa afya,” alisema Mkumbo.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Wolter Soer alisema timu yao imeridhishwa na utekelezaji wa Tasaf mkoani humo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuendeleza mpango huo. “Kwa Kabila la Wahadzabe tumeguswa zaidi, tutachukua hatua maalumu kulisaidia. Tunataka ifike wakati na Wahadzabe wawe na maisha bora kama walivyo Watanzania wengine,” alisema.

Kasango alisema Tasaf III mkoani humo imetumia zaidi ya Sh18.8 bilioni kunusuru kaya masikini 40,218, kati ya Septemba hadi Oktoba.

Hata hivyo, alisema kaya 281 zimeondolewa katika mpango huo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya kukosa sifa.