Mtalii asimulia safari ndani ya treni akivuka nchi tano hadi Tanzania

Tuesday October 17 2017

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Mtalii kutoka Uholanzi amesimulia namna alivyosafiri kutoka nchini humo hadi Tanzania kupitia Afrika Kusini alikounganisha kwa treni ya Rovos.

Zaidi ya watalii 250 wameletwa nchini na treni hiyo mwaka huu na kuanzia mwakani treni hiyo inatarajia kuongeza safari zake ikimaanisha kuimarika kwa sekta hiyo.

Mmoja wa watalii waliowasili, Bernard Fleming alisema anajisikia fahari kukanyaga ardhi ya Tanzania na anaamini Afrika ni miongini mwa maeneo salama zaidi kwa utalii na kupumzisha akili baada ya kufanya kazi muda mrefu.

“Nimetoka Uholanzi kwetu nikapitia Afrika Kusini kuja Tanzania kwa treni ya Rovos. Najisikia fahari kuwa sehemu ya abiria hawa, yapo mengi mazuri niliyosikia kuhusu nchi hii,” alisema mtalii huyo na kuongeza:

“Sijajua hasa nitatembelea vivutio gani kwa sababu naendelea kuangalia sehemu nzuri zaidi ya zote. Lakini naamini nitarejea tena Tanzania,” alisema Bernard. Mbali ya Uholanzi, mtalii huyo alipitia Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe na Zambia kabla ya kufika Tanzania. Rovos inasafirisha watalii kutoka Cape Town hadi Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Geofrey Tengeneza alisema bodi hiyo inafanya kila iwezalo kuitangaza Tanzania kimataifa kwa sababu utalii una wigo mpana.

“Kuna uhusiano mkubwa kati ya utalii na usafiri ndiyo maana tunajitahidi kuwa karibu na Tazara ili kuangalia namna ya kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vyetu,,” alisema Tengeneza.

Ofisa Uhusiano wa Reli ya Tazara, Regina Tarimo alisema imekuwa fahari kuwapokea baada ya kutumia wiki mbili safarini. “Kwa miaka kadhaa sasa tumekuwa tukiwapokea. Wakishawasili wanajigawa makundi wapo wanaoenda Zanzibar, Manyara, Selous, Ngorongoro na maeneo mengine ya vivutio,” alisema.     

Advertisement