NMB yaipa ‘mkwanja’ Alat

Muktasari:

  • Alat imesaidiwa Sh100 milioni na NMB kwa ajili ya mkutano mkuu utakaofanyika Mbeya.

Benki ya NMB imetoa hundi ya Sh100 milioni kuwezesha mkutano mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Alat), utakaofanyika Oktoba 2 hadi 6 jijini Mbeya.

Richard Makungwa, ofisa mkuu wa idara ya wateja wakubwa na Serikali wa NMB   amesema wametoa fedha hizo kuunga mkono jitihada za Alat na kuiwezesha iwajibike ipasavyo kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

"Halmashauri zipo karibu na wananchi ambao sisi tunawahudumia, kwa hiyo mchango wetu unalenga kuona malengo waliyopanga yanafikiwa," amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Alat, Steven Mhapa amesema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utahimiza halmashauri zote kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.

"Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli, mkutano huu utawahusisha pia wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya, majiji na manispaa nchini," amesema.

Amesema katika mkutano huo watatumia siku moja kuzungumzia mamlaka mpya iliyoundwa kwa ajili ya masuala ya barabara za miji na vijiji kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi.