Sekta ya benki yaanza kuona nuru mpya

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee(kushoto) akiwa katika mahojiano maalumu leo katika ofisi za Mwananchi.

Muktasari:

  • Bosi Ecobank amesema sehemu ya mikopo chechefu imeanza kulipwa

Dar es Salaam. Sekta ya benki nchini imeanza kupata matumaini ya kupunguza kiwango cha mikopo isiyolipika kutokana na kuanza kuimarika kwa biashara.

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Ecobank, Mwanahiba Mzee ameiambia Mwananchi katika mahojiano maalumu leo Alhamisi kuwa kwa miaka miwili iliyopita sekta ya benki ilipata misukosuko kidogo kutokana na wafanyabiashara kuyumba lakini sasa kuna mwelekeo chanya.

Amesema sekta ya benki iliyumba kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kucheleweshewa malipo ya kandarasi zao na kutofanya vyema kwa baadhi ya sekta muhimu kama ya gesi jambo lililofanya washindwe kurejesha mikopo kwa wakati.

Mzee aliyetembelea ofisi za Mwananchi amesema athari zozote zinazowakumba wafanyabiashara zinaathiri pia benki na sekta ya majengo, ambayo sehemu kubwa hutumika kama dhamana ya mikopo.  

Mikopo chechefu ni ile ambayo wakopaji wameshindwa kuilipa kwa taasisi za fedha ndani ya muda unaotakiwa ambao ni siku 90.

“Kandarasi nyingi bado hazijalipwa na sehemu kubwa ya dhamana za mikopo hiyo ni majengo ambayo yanashuka thamani kwa sababu wanunuzi ni wachache… hii ni hali ngumu kwa wateja,” amesema.

Amesema benki nyingi hazijapoteza fedha walizokopesha ila ni utaratibu wa kibenki unaofanya zionekane kama ni mikopo isiyolipika ilihali wanaodaiwa watailipa siku zijazo licha ya mdhibiti kutotaka kujua sababu za wateja kushindwa kulipa kwa wakati.

“Sasa hivi hata wasafirishaji waliokuwa wamepaki malori wameanza kupata biashara kwa sababu mambo yameanza kurekebishwa. Malipo ya mikopo yameanza kuja hivyo biashara nyingi zinazidi kuimarika.

“Inawezekana mwishoni mwa mwaka huu bado hali ikawa ngumu kwa sababu ndiyo wanaendelea kuimarika lakini mwakani hali itakuwa nzuri na tutaanza kuona tofauti,” amesema.

Ecobank ni miongoni mwa benki zilizokuwa na kiwango kikubwa cha mikopo chechefu kwa kuwa na asilimia 57 ya mikopo yote katika robo ya kwanza mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 38 ya robo ya mwisho wa mwaka jana.

Bosi huyo mpya amesema kazi yake kubwa kwa sasa ni kupunguza kiwango hicho cha mikopo isiyolipika ambayo imekuwa ikiisumbua benki na kuathiri faida ambayo hupatikana katika uendeshaji.

“Malengo ya Ecobank Group ni kuwa na wateja milioni 100 ifikapo 2020 lakini hapa Tanzania nataka tuwe na wateja zaidi ya milioni katika kipindi hicho na kuifanya benki iwe na faida zaidi,” amesema Mzee aliyeteuliwa kuiongoza benki hiyo kuanzia Julai.